Ngunjiri Wambugu amkosoa rais Uhuru Kenyatta kwa kutompongeza Ruto

Uhuru alikosa kumtaja wala kumpogeza naibu wake katika hotuba yake siku ya Jumatatu.

Muhtasari

•Wambugu amesema kuwa ingekuwa sawa kwa rais kumpongeza naibu huyo wake katika hotuba yake siku ya Jumatatu.

•Uhuru aliwahakikishia Wakenya kwamba ataheshimu uamuzi wa Mahakama wa kuidhinisha kuchaguliwa kwa Ruto kama rais mteule.

Mbunge wa Nyeri Mjini Ngunjiri Wambugu akiwahutubia waandishi wa habari
Mbunge wa Nyeri Mjini Ngunjiri Wambugu akiwahutubia waandishi wa habari
Image: MAKTABA

Aliyekuwa mbunge wa Nyeri Town Ngunjiri Wambugu amepinga hatua ya Rais anayeondoka Uhuru Kenyatta ya kutompongeza rais mteule William Ruto baada ya mahakama ya upeo kuidhinisha ushindi wake.

Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Wambugu amesema kuwa ingekuwa sawa kwa rais kumpongeza naibu huyo wake katika hotuba yake siku ya Jumatatu.

"Najua 6.9M kati yetu ambao hatukumpigia kura Ruto tumekasirika sana. Lakini kwa heshima ya 7.1M ambao IEBC inasema walimpigia kura Ruto, na kusaidia Kenya kusonga mbele kama taifa moja la umoja usiogawanyika, Uhuru alipaswa kumpongeza Ruto jioni hii," Wambugu alisema Jumatatu jioni.

Haya yalijiri muda mfupi baada ya mbunge huyo wa zamani ambaye kwa kipindi kirefu amekuwa mkosaoji mkubwa wa Ruto kumpongeza kwa ushindi wake katika kinyang'anyiro cha urais cha mwaka huu.

Katika ujumbe wake wa pongezi, Wambugu  alimtakia rais mteule heri anapochukua jukumu lake mpya la kuongoza nchi ya Kenya na kumtaka atimize ahadi ambazo alitoa kwa Wakenya wakati wa kampeni.

Hongera Rais William Ruto. Umeshinda dhidi ya uwezekano mkubwa sana. Sasa ninaomba kwa dhati ufanikiwe unapoliongoza taifa letu kuu la Kenya mbele. Sasa tunakusubiri kwa hamu #TimizaAhadi," aliandika.

Wambugu ni miongoni mwa viongozi wa eneo la Mt Kenya ambao walitia juhudi kubwa katika kumpigia debe mgombea urais wa Azimio Raila Odinga.

Mwezi uliopita, wengi wa viongozi hao waliishia kupoteza viti vyao katika uchaguzi wa Agosti 9. Ngunjiri,  Jeremiah Kioni, Amos Kimunya, Kiraitu Murungi, Ephraim Maina na Kanini Kega ni baadhi tu ya  wahanga wa 'Wimbi la UDA'  katika eneo hilo linaloaminika kuwa ngome ya UDA.

Jumatatu jioni rais Uhuru Kenyatta aliwahakikishia Wakenya kwamba ataheshimu uamuzi wa Mahakama ya Upeo wa kuidhinisha kuchaguliwa kwa naibu wake, William Ruto kama rais mteule.

Katika video iliyochapishwa kwenye ukurasa rasmi wa Ikulu ya Kenya, Uhuru alitoa hakikisho kuwa mchakato wa kupitisha mamlaka utaendelea vizuri na kubainisha kwamba matayarisho tayari yameanza.

"Leo, Mahakama ya Upeo zaidi ilifanya uamuzi kuhusu mzozo wa urais unaodumisha matokeo yaliyotangazwa na IEBC. Katika kutimiza ahadi niliyotoa ya kuzingatia sheria, ninajitolea kutekeleza maagizo ya mahakama," alisema.

Rais hata hivyo hakumtaja naibu wake wala kumpongeza katika taarifa hiyo yake, jambo ambalo limeibua hisia mseto nchini.