Viongozi wa Azimio wakamatwa wakiongoza maandamano Nairobi, baadhi wazuiwa kuondoka nyumbani

Seneta Stewart Madzayo na mbunge mwingine mwanamke ni miongoni mwa waliokamatwa.

Muhtasari

•Viongozi wawili wa upande wa upinzani  na waandamanaji kadhaa wametiwa mbaroni kwa kuongoza maandamano katikati mwa Jiji la Nairobi.

akamatwa wakati wa maandamano ya Azimio katika KICC mnamo Machi 20, 2023.
Kiongozi wa wachache katika Seneti Stewart Madzayo akamatwa wakati wa maandamano ya Azimio katika KICC mnamo Machi 20, 2023.
Image: EZEKIEL AMINGA

Viongozi wawili wa upande wa upinzani  na waandamanaji kadhaa wametiwa mbaroni kwa kuongoza maandamano katikati mwa Jiji la Nairobi.

Kiongozi wa wachache katika seneti, Stewart Madzayo na mbunge mwingine mwanamke ni miongoni mwa waliokamatwa.

Viongozi hao waliingia katika KICC Siku ya Jumatatu asubuhi wakiandamana na kundi la waandamanaji. Mara tu baada ya kuingia walifukuzwa na maafisa wa polisi ambao waliwarushia vitoa machozi.

Haijulikani wawili hao walipelekwa wapi baada ya kuwekwa ndani ya gari la polisi. Kundi la waandamanaji pia walikamatwa wakati wa maandamano ya Jumatatu asubuhi.

Maandamano ambayo yaling'oa nanga jijini Nairobi siku ya Jumatatu asubuhi yaliitishwa na kiongozi wa Azimio, Raila Odinga.

akamatwa wakati wa maandamano ya Azimio katika KICC mnamo Machi 20, 2023.
Mbunge akamatwa wakati wa maandamano ya Azimio katika KICC mnamo Machi 20, 2023.
Image: EZEKIEL AMINGA
 

Vigogo kadhaa wa Azimio wamezuiwa kuondoka makwao huku kiongozi wa Azimio Raila Odinga akiwa bado haijulikani aliko.

Kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua, ambaye alikuwa mgombea mwenza wa Raila katika uchaguzi wa urais mwaka jana, ni miongoni mwa walioathirika.

Inasemekana alilala nyumbani kwake lakini hakuweza kutoka nje ya boma huku polisi wakiwa wamefunga barabara.

Haijabainika ni wapi Raila alilala usiku huku shughuli ndogo ikionekana kwenye barabara inayoelekea nyumbani kwake Karen.

Hata hivyo, Raila ameandika ujumbe kwenye Twitter akisema kuwa yuko njiani kuelekea mjini.

"Naona Kazi Imeanza tuko njiani nasi. #DateWithDestiny20thMarch," alitweet akiambatanisha na video ya viongozi katika KICC.

Baadhi ya wabunge tayari wameandaa maandamano katika KICC huku polisi wakiwakamata waandamanaji kadhaa.

Viongozi wa Azimio wanatarajiwa kuongoza maandamano katikati mwa jiji na kuendelea hadi Ikulu ili "kurudisha ushindi wao ulioibiwa".