Wapelelezi kufukua mwili wa Jeff Mwathi, Bosi wa polisi aeleza kwa nini

Marehemu Jeff alizikwa nyumbani kwao Nakuru mnamo Machi 3.

Muhtasari

•Koome alisema wamepata mapengo katika tukio hilo na hivyo wanahitaji kuufukua mwili wa marehemu ili kusaidia katika uchunguzi wao.

•IG Koome alionya kuwa yeyote atakayepatikana na hatia ya mauaji hayo atakabiliwa na mkono wa sheria.

Marehemu Jeff Mwathi na DJ Fatxo
Image: HISANI

Wapelelezi wanapanga kuufukua mwili wa marehemu Geoffrey Jeff Mwathi kama sehemu ya uchunguzi unaoendelea kuhusu kifo chake.

Jumapili, Inspekta Jenerali wa polisi Japhet Koome alisema wamepata mapengo katika tukio hilo na hivyo wanahitaji kuufukua mwili wa marehemu ili kusaidia katika uchunguzi wao.

Alisema polisi wanaendelea na uchunguzi wa kina ili kuhakikisha haki inatendeka katika kesi hiyo.

"Tutafukua mwili huo kwa kuangalia vipimo vya mahali ambapo inasemekana alipita kwenye dirisha na kushuka hadi ghorofa ya chini. Tunaelekea kortini kutafuta agizo la uchimbaji wa kaburi hilo,” Koome alisema.

IG alibaini kuwa Jeff alizikwa zamani nyumbani kwao Nyandarua na hivyo kuna haja ya kutafuta agizo la kuufukua mwili huo.

Koome alizungumza katika afisi yake jijini Nairobi na kuonya yeyote atakayepatikana na hatia ya mauaji hayo atakabiliwa na mkono wa sheria.

"Yeyote atakayepatikana na hatia atawajibishwa," alisema.

Haya yanajiri baada ya maafisa wa upelelezi kutoka Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kusema wanaamini Jeff aliuawa kabla ya mwili wake kutupwa nje.

Wapelelezi wa mauaji wanaoshughulikia kesi hiyo kutoka kwa uchunguzi wao, kijana huyo mwenye umri wa miaka 23 aliuawa wala hakuruka kutoka kwa ghorofa hadi kufa kama ilivyoripotiwa hapo awali.

Awali iliripotiwa alifariki kwa kujitoa uhai katika tukio la Februari 22.

Baada ya wapelelezi kuzuru eneo la tukio kwa ajili ya ujenzi upya na uchunguzi wa kitaalamu waligundua dalili za mapambano ndani ya nyumba ya mwanamuziki wa Mugithi Lawrence Njuguna almaarufu DJ Fatxo.

Baadhi ya vifaa vya muziki vilipatika vimevunjwa ndani ya nyumba kutokana na mapambano, maafisa wanasema.

Wapelelezi walidokeza kuwa kulikuwa na uwezekano wa vita kabla ya Jeff kuvutwa nje na kutupwa kutoka juu ya paa au kutoka ngazi za ghorofa ya 12.

Wachunguzi, wakitupilia mbali madai ya kujitoa uhai, wanaamini kuwa Jeff aliuawa kabla ya kutupwa mbali ili kuficha ukweli na kuifanya ionekane kama kujiua.

Hapo awali, ilirekodiwa kwamba Jeff aliruka kutoka kwenye dirisha la chumba cha kulala, lakini hiyo ilikataliwa kwani haiwezekani kwa mtu mzima kuingia kwenye fremu za dirisha zilizobana za dirisha.

Wapelelezi wa mauaji walisema mchakato wa upelelezi ni pamoja na kuwahoji kundi la kwanza la mashahidi katika kesi hiyo, uchunguzi wa eneo la tukio na kupata picha za CCTV zilizonasa dakika za mwisho za marehemu.

Maafisa wa upelelezi walisema sasa wanaendelea na awamu ya pili ya uchunguzi ambapo watu kadhaa waliohusishwa watahojiwa na mapendekezo mwafaka yatatolewa kwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (ODPP).

Wapelelezi walisema watu watakaohojiwa katika awamu inayofuata watajumuisha watu wote watano waliokuwa nyumbani kwa DJ Fatxo wakati tukio hilo likitokea.

Pia wa kuhojiwa, kulingana na DCI, ni maafisa wa polisi walioshughulikia kesi hiyo kwanza.