Hatimaye ninaweza kumnunulia baba yangu gari-Faith Kipyegon asema baada ya tuzo ya Ksh.5M kutoka kwa Serikali

Kipyegon alivunja Rekodi mbili za Dunia katika muda wa wiki moja kwenye Ligi ya Diamond huko Florence, Italia na Paris,

Muhtasari
  • Aidha, bingwa huyo wa mbio za marathoni alizawadiwa nyumba mpya yenye thamani ya Ksh.6 milioni iliyoko katika eneo la Park Road Nairobi.
MWANARIADHA FAITH KIPYEGON NA RAIS WILIAM RUTO
Image: TWITTER

Mwanariadha wa mbio za juu Faith Kipyegon sasa anasema hatimaye anaweza kumnunulia babake gari jipya hii ni baada ya Rais Ruto kumtunuku zawadi ya milioni 5.

Kipyegon aliyekuwa akitokwa na machozi alifichua hayo alipokuwa akihutubia katika Ikulu ya Nairobi siku ya Jumanne ambapo alikaribishwa na Rais William Ruto kusherehekea mafanikio yake ya hivi majuzi kwenye mashindano hayo.

Kipyegon alivunja Rekodi mbili za Dunia katika muda wa wiki moja kwenye Ligi ya Diamond huko Florence, Italia na Paris, Ufaransa; alikimbia mbio za 1500M kwa muda wa 3:49.11 na 5000M kwa 14:05.20.

Kufuatia hili, Rais Ruto alisema serikali kuanzia sasa itamtuza mwanariadha yeyote - kuanzia na Kipyegon - ambaye atavunja rekodi ya dunia kwa Ksh.5 milioni pesa taslimu.

Kipyegon aliendelea kueleza kuwa alikuwa ameahidi kumzawadia babake mzee gari jipya iwapo angevunja rekodi ya dunia; ahadi ambayo anasema sasa ataweza kutimiza, kwa zawadi ya pesa taslimu kutoka kwa serikali.

“Asante sana Mheshimiwa Rais. Nimefurahishwa sana na malipo hayo, sasa ninaweza kumiliki nyumba Nairobi, na kwa pesa ninazoweza kusema sasa ninaweza kumnunulia babangu gari. Nilimuahidi kwamba ningevunja Rekodi ya Dunia kwamba ningemnunulia gari...sasa naweza kutimiza ahadi yangu,” alisema Kipyegon mwenye hisia kali, katikati ya machozi.

Aidha, bingwa huyo wa mbio za marathoni alizawadiwa nyumba mpya yenye thamani ya Ksh.6 milioni iliyoko katika eneo la Park Road Nairobi.