Faith Kipyegon afichua siri kubwa nyuma ya mafanikio yake makubwa mwaka huu

Kipyegon alisema kuwa mazoezi ya mbio za masafa marefu imekuwa sehemu ngumu zaidi ya matayarisho yake.

Muhtasari

•Kipyegon alifichua kwamba amekuwa akiamka asubuhi sana na kufanya mazoezi kwa bidii huku akijiandaa kwa mbio hizo.

•Faith alisema anapenda zaidi mbio za mita 1500 kwani amekuwa akijituma zaidi katika mbio hizo kwa miaka kadhaa.

Faith Kipyegon
Faith Kipyegon
Image: HISANI

Bingwa wa Dunia katika mbio za mita 1500 na 5000, Faith Kipyegon amefichua kuwa sababu kuu ya mafanikio yake makubwa mwaka huu imekuwa bidii na mazoezi ya kujitolea.

Akizungumza na mwanahabari, mwanariadha huyo wa Kenya mwenye umri wa miaka 29 alifichua kwamba amekuwa akiamka asubuhi sana na kufanya mazoezi kwa bidii huku akijiandaa kwa mbio hizo.

"Nadhani sababu kuu imekuwa mazoezi. Kuamka mapema na kufanya mazoezi, nikilenga msimu bora zaidi,” Faith alisema.

Mshikilizi wa rekodi ya dunia katika mbio za mita 1500 na 5000 alisema kuwa mazoezi ya mbio za masafa marefu imekuwa sehemu ngumu zaidi ya matayarisho yake.

“Siipendi sana. Lakini yote inahusu kukabiliana, kuamka na kusonga mbele, " alisema.

Faith alisema anapenda zaidi mbio za mita 1500 kwani amekuwa akijituma zaidi katika mbio hizo kwa miaka kadhaa.

"Hiyo (mita 1500) ni mtoto wangu kwa sababu nimekuwa nikitazamia rekodi hiyo ya dunia kama miaka mitatu iliyopita na sikufanikiwa. Lakini mwaka huu nimefanikiwa,” alisema.

Wiki iliyopita, Faith Kipyegon alijishindia dhahabu mbili baada ya kuibuka wa kwanza katika mbio za mita 1500 na 5000 katika mashindano ya Dunia yaliyokamilika mjini Budapest, Hungary.

Siku ya Jumamosi, Kipyegon alidhibitisha hadhi yake kama mmoja wa magwiji wa wakati wote kwa kushinda mara mbili  katika mji mkuu wa Hungary.

Baada ya kushinda taji la tatu la dunia la mbio za mita 1,500 siku ya Jumanne, Kipyegon aliwasilisha dhahabu nyingine, wakati huu katika mbio za mita 5,000.

Mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 29 alijitolea muda wake na akapata ushindi kwa dakika 14, sekunde 53.88.

Katika taarifa ya siku ya Jumapili, Kipyegon alisema amekuwa na msimu bora.

"Huu umekuwa mwaka wa ajabu kwangu. Kuweka historia jana, kushinda medali mbili za dhahabu katika mashindano ndio nilikuwa nikitamani msimu huu," alisema.

"Ndoto yangu ilitimia, inashangaza. Nimekuwa thabiti, nikizingatia mstari wa kumaliza na kuandika historia," Kipyegon aliongeza.

Kipyegon aliapa kuendelea kujitutumua katika siku zijazo.

Alitoa shukrani kwa Wakenya kwa kumuunga mkono, haswa bintiye.

"Binti yangu ananipa sapoti ya ajabu, huwa ananiambia naweza kufanya hivyo. Mwisho kabisa, nataka kuishukuru timu yangu ya thamani, kocha wangu, usimamizi wangu na mashabiki wote wa ajabu!" Kipyegon aliongeza.