Phil Foden na Cole Palmer washinda tuzo za wachezaji bora wa msimu ligini EPL

Wakati Foden anatajwa kuwa mshindi wa tuzo ya mchezaji bora wa msimu, Palmer alijishindia tuzo ya mchezaji bora chipukizi katika ligi hiyo ya premia, wote wakiwa wahitimu wa akademia ya Man City kabla ya Palmer kutimukia Chelsea.

COLE PALMER na PHIL FODEN
COLE PALMER na PHIL FODEN
Image: HISANI

Phil Foden wa Manchester City ameshinda tuzo ya mchezaji bora wa ligi ya premia huku mwenzake wa Chelsea Cole Palmer akishinda tuzo ya mchezaji bora chipukizi katika ligi hiyo.

Foden mwenye umri wa miaka 23, ambaye ana mabao 17 na asisti nane msimu huu kwa viongozi wa sasa wa Ligi ya Premia Manchester City, pia alichaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Waandishi wa Soka mapema mwezi huu.

Foden alikuwa mshindi mara mbili wa tuzo ya Mchezaji Bora Chipukizi wa Ligi ya Premia mnamo 2021 na 2022 na aliteuliwa kuwania tuzo kuu pamoja na Erling Haaland, Alexander Isak, Martin Odegaard, Cole Palmer, Declan Rice, Virgil Van Dijk na Ollie Watkins mwaka huu.

Kwa upande mwingine, Cole Palmer alichaguliwa kuwa Mchezaji Chipukizi wa Hublot 2023/24.

Kiungo mshambuliaji Palmer amekuwa na kampeni ya kuvutia tangu ajiunge na Chelsea kutoka Manchester City msimu uliopita wa joto.

Palmer, aliyefikisha umri wa miaka 22 wiki iliyopita, amefunga au kusaidia mabao 32 msimu huu, idadi kubwa zaidi ya mchezaji yeyote katika Ligi Kuu ya Uingereza.

Ni mchezaji wa tatu pekee katika historia kufikisha mabao 30+ katika msimu wa PL akiwa na umri wa miaka 21 au chini, baada ya Robbie Fowler na Chris Sutton.