Baada ya vipimo vya afya, Mandonga apatikana yuko sawa na kuondolewa marufuku ya kupigana

Kamisheni hiyo ilitaka Mandonga ambaye amekuwa anapigana mapambano mfululizo apimwe hasa maeneo ya kichwani ili kuona utimamu wake kiafya.

Muhtasari

• Kamisheni hiyo sasa inadaiwa kuridhishwa na taarifa za daktari kwamba bondia huyo mwenye tambo nyingi yuko katika hali sawa.

Karim Mandonga
Karim Mandonga
Image: Instagram

Siku chache zilizopita, taaria kutoka kwa shirika la habari la Zanzibar ZBC ziliripoti kwamba kamisheni inayosimamia mchezo wa ngumi za kulipwa Tanzania TPBRC ilitoa wasiwasi wake kuhusu afya ya bondia Karim Mandonga na kumpiga marufuku kushiriki mchezo huo hadi pale atakapofanyiwa vipimo vya afya.

Kamisheni hiyo sasa inadaiwa kuridhishwa na taarifa za daktari kwamba bondia huyo mwenye tambo nyingi yuko katika hali sawa ya kupambana wakati wowote.

Kwa mujibu wa George Silasi Lukindo, Katibu Mkuu wa Kamisheni ya Ngumi za kulipwa Tanzania (TPBRC), Matokeo ya uchunguzi wa kitabibu yaliyofanyika juzi yanaonyesha kuwa Mandonga hajaathirika katika maeneo yaliyofanyiwa uchunguzi.

"Ushiriki wa bondia kwa muktadha wa majadiliano yetu ni lazima athibitishwe utamamu wake wa afya ya mwili na chombo chenye mamlaka ya kufanya vipimo hivyo", Lukindo ameiambia BBC.

Kwa mujibu wa Lukindo suala la afya ni muhimu kwa bondia kwa sababu uwajibikaji zaidi unakuwa kwa bondia husika kama masharti yamezingatiwa.

"Hakuna wa kuwajibishwa kuhusiana na afya ya bondia ikiwa vigezo na masharti ya ushiriki wake kwenye mchezo husika vimefuatwa kikamilifu", alisema.

Kamisheni hiyo ya kusimamia ndondi za kulipwa Tanzania ilichukua uamuzi wa kumsimamisha Mandonga kutokana na wasiwasi na hali yake ya afya kufuatia kipigo alichopata kutoka kwa Moses Golola aliyemshinda kwa Technical Knock Out Julai 29, 2023 jijini Mwanza.

Wiki moja kabla ya pambano hilo, Julai 22, 2023 Mandonga alitoka kupigwa na Mkenya Daniel Wanyonyi.

Kamisheni hiyo ilitaka Mandonga ambaye amekuwa anapigana mapambano mfululizo apimwe hasa maeneo ya kichwani ili kuona utimamu wake kiafya.