Mandonga akubali kichapo cha pili ndani ya wiki, "Atake atapigwa, asitake atapigwa tu!"

Mandonga alianza pambano hilo kwa tambo zake za vitisho huku mashabiki wa nyumbani wakimshabikia lakini Mganda Golola aliyetulia alimpiga na kumuangusha katika raundi ya tatu "Technical Knock Out"

Muhtasari

• Licha ya kufanya pambano kali, alizidiwa nguvu na Golola, ambaye hatimaye alimtoa katika raundi ya tatu.

• Ushinde huu unakula wiki moja tu baada ya kuchabangwa Nairobi na Daniel Wanyonyi.

Mandonga apigwa tena
Mandonga apigwa tena
Image: Screenrab

Mwezi wa Julai unapokamilika, si mwezi ambao mwanamasumbwi kutoka Tanzania Karim Mandonga almaarufu Mtu Kazi atataka kukumbuka kabisa katika maisha yake.

Huu ni mwezi ambao bondia huyo ameshindwa kuibuka mshindi kwenye ulingo wa ndondi, ukiwa ni msururu mbaya kabisa wa matokeo kabisa taaluma hiyo yake.

Ikiwa ni wiki moja tu baada ya kupewa kichapo kikali ulingoni na bondi wa Kenya Daniel Wanyonyi jijini Nairobi, bondia huyo mbwatukaji alirejea nchini kwao na kujifua akiwa na matumaini ya kujirudi katika fomu yake ya kushinda.

Kwa bahati mbaya, Jumamosi usiku tena alikabidhiwa kupigo kikali mbele ya mashabiki wa nyumbani jijini Mwanza na bondia wa Uganda Moses Golola katika pambano ambalo lilipeperushwa moja kwa moja kwenye runinga ya Azam.

Licha ya kufanya pambano kali, alizidiwa nguvu na Golola, ambaye hatimaye alimtoa katika raundi ya tatu, na kupata ushindi mnono kwenye Technical Knock Out.

Wiki moja tu mapema, Jumamosi, Julai 22, Mandonga alikumbana na misukosuko mingine alipopambana na bondia Mkenya Daniel Wanyonyi.

Hata hivyo, hii ilikuwa kama kulipiza kwa Wanyonyi ambaye alichapwa na bondia huyo mwenye kidomo mnamo Januari mwaka huu katika pambano lililoandaliwa kwenye ukumbi wa kimataifa wa KICC jijini Nairobi.

Baada ya ushindi huo wa Mandonga, alijitapa vikali akirudi nchini kwao na kuzawadiwa gari na mhisani mmoja miongoni mwa zawadi nyingine nyingi.

Bondia huyo amesifiwa vikali kwa kuleta uhai katika mchezo wa ngumi kwenye ukanda wa Afrika Mashariki kutokana na tambo zake ambazo zinawavutia mashabiki na wapenzi wa ndondi kwenye ukanda huu ambao haujaonekana kukumbatia mchezo huo kwa miaka mingi sasa.