Harambee Stars yanyolewa bila maji na Mali, 5-0

Muhtasari

•Harambee Stars ililazwa mabao matano bila jawabu na wenyeji wake Mali mida ya saa nne usiku wa Alhamisi.

•Kwa sasa Mali inaongoza kundi E na pointi 7, Uganda imeshikilia nafasi ya pili na pointi 5 baada ya kushinda Rwanda 1-0 usiku wa Alhamisi, Harambee Stars ya tatu na pointi mbili huku Rwanda ikifunga mkia katika kundi hilo na pointi moja.

Image: FACEBOOK// HARAMBEE STARS

Ndoto za timu ya taifa Harambee Stars za kushiriki kwenye Kombe la dunia mwaka ujao zimeendelea kufifia baada ya kupoteza kwenye mechi ya tatu katika hatua ya makundi.

Usiku wa Alhamisi utabaki kuwa usiku wa kusahau kwa Harambee Stars kufuatia matokeo mabaya  ambayo yaliandikishwa ugani Stade Adrar nchini Mali.

Harambee Stars iliangamizwa vibaya kwa kulazwa mabao matano bila jawabu na wenyeji wake Mali mida ya saa nne usiku wa Alhamisi.

Hattrick ya mshambulizi Ibrahima Kone na mabao mawili ya Adama Traore na  Moussa Doumbia yalifanikishia wenyeji kupata ushindi huo mkubwa wa kujivunia.

Harambee Stars ilisonga katika nafasi ya tatu kwenye kundi E ikiwa imezoa pointi mbili tu kutoka kwa mechi tatu ambazo  tayari zimechezwa.

Mechi za awali dhidi ya Uganda na Rwanda ziliishia sare ya 0-0 na 1-1 mtawalia.

Kwa sasa Mali inaongoza kundi E na pointi 7, Uganda imeshikilia nafasi ya pili na pointi 5 baada ya kushinda Rwanda 1-0 usiku wa Alhamisi, Harambee Stars ya tatu na pointi mbili huku Rwanda ikifunga mkia katika kundi hilo na pointi moja.

Timu moja tu itahitimu kuingia kwenye raundi ya tatu ya kufuzu kushiriki katika kombe la dunia baada ya msimu kuisha.