"Hatutasajili wachezaji wa Kiafrika tena!" Rais wa klabu ya Napoli, Aurelio De Laurentiis

Rais huyo alisema iwapo watawaajili basi sharti wachezaji hao wawe tayari kuasi kushiriki kipute cha AFCON kwa mataifa yao.

Muhtasari

• Rais huyo alisema huwa hawapatikani kuitumikia timu wakati wanapoyawakilisha mataifa yao katika kipute cha AFCON.

• Alisema klabu ndio wajinga kuendelea kuwalipa mishahara minono ya kuwazungusha duniani bila kuichezea timu wakati inawahitaji.

Rais wa klabu ya Napoli, Aurelio De Laurentiis
Rais wa klabu ya Napoli, Aurelio De Laurentiis
Image: Twitter//Aurelio De Laurentiis

Taarifa kutoka Italy katika klabu ya Napoli si nzuri sana kwa wachezaji wa kimataifa kutoka bara la Afrika.

Hii ni baada ya rais wa klabu hiyo kutangaza kwamba katika siku za mbeleni hawezi tena kubali klabu yake kuwasajili wachezaji kutoka mataifa ya Afrika.

Rais Aurelio De Laurentiis alisema kwamba klabu ya Napoli itakuwa ikiwaandikisha mikataba wachezaji kutoka Afrika iwapo tu watatia nadhiri tena kwa njia ya maandishi kwamba pindi watakapojiunga na klabu hiyo basi wanaasi kuchezea mataifa yao katika kipute cha AFCON.

“Niliwaambiwa vijana hao kwamba wasiwahi kunizungumzia kuhusu Waafrika tena. Mimi nawapenda, lakini ni iwapo watakula Yamini kwa njia ya maandishi kwamba hawatoshiriki katika kipute cha AFCON ama kingine kati ya mashindano hayo, mashindano ya kufuzu kipute cha ubingwa wa dunia kule Amerika ya Kusini, wachezaji hawa huwa hawapatikani,” rais Aurelio De Laurentiis alitema moto.

Alizidi kusema kwamba klabu ya Napoli ndio wajinga wa kuendelea kuwalipa mishahara minono ya kuwawezesha kusafiri kote duniani kuwajibikia mataifa yao katika mashindano mbalimbali.

Itakumbukwa kwamba katika kipute cha AFCON mwaka 2021 amabcho kilikamilika miezi michache iliyopita ambapo Senegali ilitawazwa mabingwa, Klabu ya Napoli ilitishia kushtaki mataifa ya Afrika ambayo yalikuwa yakiwataka wachezaji wake kuyawakilisha kutoka klabu hiyo. Wachezaji hao walikuwa ni mshambuliaji Victor Osimhen kutoka Nigeria, beki Kalidou Koulibaly kutoka Senegal, Anguissa Andre Zambo miongoni mwa wengine.

Taarifa hizi bila shaka zitawaathiri sana wachezaji wengi wa Kiafrika waliokuwa na ndoto ya kuisakatia klabu hiyo ya Italia huku pia wachezaji kama Victor Osimhen na Anguissa Zambo ambao bado wanaisakatia klabu hiyo wakiwa katika hali ya sintofahamu kutokana na taarifa hiyo ya rais wa klabu.

Mapema wiki jana, mwafrika mwenzao, beki Kalidou Koulibaly aligura klabu hiyo na kujiunga na miamba wa Uingereza, Chelsea kwa mkataba wa miaka mitatu.

Sasa mataifa mengi ya Afrika na wapenzi wa soka la ulaya na kipute cha AFCON wakibaki katika njia ya kushika tama, matumaini yao makubwa yakiwa ni kuomba vilabu vingine Uropa visichukue hatua kama hizo za Napoli za kuwakataa wachezaji wa Kiafrika na kuwashrutisha wale walioko kwenye timu zao kuasi kuwakilisha mataifa yao kama njia moja ya kupata nafasi kwenye klabu.