Mbappe akanusha uvumi kuwa hana furaha katika klabu ya PSG na anataka kuondoka

Nilitaka tu kusema kwamba sio kweli kabisa - Mbappe.

Muhtasari

• Alisema kwamba alishtushwa na uvumi huo ambao si wa kweli uliokuwa unamhusisha na taarifa za kutaka kuondoka Januari.

Mbappe akanusha kutaka kuondoka PSG
Mbappe akanusha kutaka kuondoka PSG
Image: Maktaba

Mshambuliaji wa PSG, Kylian Mbappé amekanusha ripoti kwamba anataka kuondoka katika klabu hiyo ya ligi ya Ufaransa wakati wa dirisha la usajili la Januari.

Wiki moja iliyopita, kulikuwepo na minong’ono mingi mitandaoni na majarida ya spoti nchini Ufaransa na Uhispania ikisemekana kwamba Mbappé hana furaha tena katika klabu hiyo na alikuwa anatafuta njia ya kuondoka katika dirisha dogo la uhamisho wa wachezaji mwezi Januari.

Mshindi huyo wa Kombe la Dunia alisema alishangazwa na uvumi huo ulipoibuka wiki iliyopita kabla ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa.

"Nina furaha sana, sijawahi kuomba kuondoka Januari," Mbappé aliwaambia waandishi wa habari katika uwanja wa Parc des Princes baada ya PSG kuishinda Marseille 1-0 Jumapili.

“Baadhi ya watu wanaweza kudhani nilihusika katika hili, lakini sikuhusika hata kidogo. Nilishtuka kama mtu mwingine yeyote ... nilitaka tu kusema kwamba sio kweli kabisa,” Mfaransa huyo aliweka wazi.

Mbappé alikuwa karibu kujiunga na Real Madrid kwa uhamisho wa bure msimu huu wa joto lakini hatimaye alikubali kusalia PSG kwa miaka miwili zaidi na chaguo la msimu wa ziada.

Mbappé alijiunga na PSG kutoka Monaco mwaka 2017 alipokuwa bado kijana. Mara nyingi amesema kuwa kuichezea Madrid ilikuwa ndoto yake ya utotoni.

Hata alipotia saini nyongeza yake, Mfaransa huyo hakufutilia mbali uwezekano wake wa kuhama siku moja, labda mkataba wake na miamba hao wa Ufaransa utakapokamilika.