Ronaldo de Lima ndio 'GOAT' wa soka, Messi na C. Ronaldo hawana lolote jipya - Mourinho

Alikiri kuwa japo Messi na CR7 wamekuwa katika viwango vya juu kwa muda, lakini katika talanta hawamfikii Nazario.

Muhtasari

• “Ronaldo, ni gwiji kuliko mtu yeyote," Mourinho alitamka alipoulizwa na Livescore kwamba anadhani GOAT wa soka ni nani.

Mourinho ataja GOAT wake katika soka
Mourinho ataja GOAT wake katika soka
Image: Getty Images

Kocha mbwatukaji Mreno Jose Mourinho amefunguka kuwa kulingana na yeye na tajriba aliyo nayo katika malimwengu ya soka kwa miongo kadhaa, katu hawezi kuwachagua Mreno mwezake Christiano Ronaldo wala Muargentina Lionel Messi kama wafalme wa soka duniani katika Karne hii.

Mourinho badala yake alimtaja mshambuliaji mkongwe wa Brazili Ronaldo de Lima kama mchezaji aliyetawala saka malimwengu ya soka kwa ustadi wake uwanjani kuwaliko Messi na Ronaldo.

Meneja huyo ambaye ameshinda mataji mengi akiwa na timu mbalimbali za bara Ulaya kwa sasa anainoa timu ya AS Roma inayoshiriki ligi ya Serie A nchini Italia.

Kwa muda mrefu zaidi ya miaka 15 sasa, Ronaldo wa Ureno na Messi wamekuwa wakilinganishwa katika mijadala mbalimbali kuhusu ni nani mfalme wa soka katika karne hii.

Lakini kwake Mourinho, wawili hao hata hawafikii robo ya umahiri wa Ronaldo Nazario de Lima wa Brazil.

“Ronaldo, ni gwiji kuliko mtu yeyote," Mourinho alitamka alipoulizwa na Livescore kwamba anadhani GOAT wa soka ni nani.

Hata hivyo, Mreno Jose Mourinho alikiri kwamba Ronaldo (CR7) na Messi wamekuwa wachezaji wa muda mrefu zaidi katika viwango vya juu kwa miaka mingi lakini akasema ikija ni masuala ya kuchanganua vilivyo upande wa kipaji cha kusakata kaumbu basi hakuna anayemfikia de Lima.

"Walakini, ikiwa tunazungumza kwa ukali kuhusu talanta na ustadi, hakuna mtu anayemzidi Ronaldo [Nazario]," aliongeza.