Ligi za soka Uturuki yasitishwa baada ya rais wa timu kumpiga ngumi mwamuzi - video

Refa huyo alishambuliwa baada ya kuongeza dakika 7 kwenye mchezo na kupelekea timu pinzani kufunga bao la kusawazisha dakika ya 97.

Muhtasari

• Mwamuzi wa FIFA tangu 2017, Meler mwenye umri wa miaka 37 alisimamia mchezo wa makundi wa Ligi ya Mabingwa wa Lazio dhidi ya Celtic mnamo Novemba 28.

Refa wa ligi ya Uturuki ashambuliwa
Refa wa ligi ya Uturuki ashambuliwa
Image: Screengrab//Video

Shirikisho la Soka la Uturuki (TFF) limesimamisha ligi zote katika usiku wa "aibu" kwa soka la taifa hilo baada ya rais wa klabu ya Ankaragucu, Faruk Koca kumpiga ngumi usoni mwamuzi mwishoni mwa mechi yao ya nyumbani ya Super Lig dhidi ya timu ya Rizespor.

Koca aliingia uwanjani na kumgonga mwamuzi Halil Umut Meler wakati filimbi ya mwisho ilipopulizwa baada ya Rizespor kufunga bao la kusawazisha dakika ya 97 katika sare ya 1-1 Uwanja wa Eryaman siku ya Jumatatu, kanda za shirika la utangazaji la TRT zilionyesha.

Mashabiki wa Ankaragucu walivamia uwanja baada ya mchezo na Meler pia alipigwa teke alipoanguka, ingawa haikujulikana washambuliaji wake walikuwa nani. Hatimaye Meler alifika kwenye chumba cha kubadilishia nguo kwa usaidizi wa polisi.

"Shirikisho la Soka la Uturuki limeamua kusimamisha michezo yote katika ligi zote kwa muda usiojulikana," shirikisho hilo liliandika kwenye X, ambayo zamani ilijulikana kama Twitter.

"Klabu husika, mwenyekiti wa klabu, viongozi wa klabu na wote walio na hatia ya kumshambulia mwamuzi Umut Meler wataadhibiwa kwa masharti makali zaidi."

Amri ya kuzuiliwa kwa Koca imetolewa, Waziri wa Mambo ya Ndani Ali Yerlikaya alisema katika chapisho kwenye X, na kuongeza kuwa watu wawili tayari wamezuiliwa kama sehemu ya uchunguzi wa mahakama juu ya tukio hilo, kulingana na shirika la habari la Reuters.

"Soka la Uturuki limepigwa ngumi ya aibu usiku huu. Kila aliyehusika katika tukio hili atalipa gharama," Mwenyekiti wa TFF Mehmet Buyukeksi alisema, kwa mujibu wa TRT.

Mwamuzi wa FIFA tangu 2017, Meler mwenye umri wa miaka 37 alisimamia mchezo wa makundi wa Ligi ya Mabingwa wa Lazio dhidi ya Celtic mnamo Novemba 28.

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alitweet: "Michezo ina maana ya amani na udugu. Michezo haiendani na vurugu. Kamwe hatutaruhusu vurugu kutokea katika michezo ya Uturuki."

Waamuzi nchini Uturuki mara nyingi hukosolewa na wasimamizi wa vilabu na marais kwa maamuzi yao lakini mara chache huwa wanalengwa na mashambulizi makali.

 

Ankaragucu iko katika nafasi ya 11 kwenye msimamo kwa pointi 18, nafasi tatu chini ya Rizespor kwa pointi 22 baada ya mechi 15.