Jirani kafanyaje? Masaibu kambini Taifa Stars ya Tanzania, kocha akitupiwa virago

Kufuatia matamshi hayo ya uchochezi kwamba Morocco wanapanga matokeo kwa kujichagulia waamuzi katika mechi zao, CAF ilimpata na hatia raia huyo wa Algeria na kumpiga faini ya dola elfu 10 [Ksh 1,617,500].

Muhtasari

• Tanzania kwa sasa wanajiandaa kwa mechi yao ya pili kwenye kundi lao dhidi ya Zambia baada ya kupoteza mechi ya kwanza mikononi mwa Morocco mabao 3-0.

Adel Amrouche asimamishwa kazi na TFF ya Tanzania.
Adel Amrouche asimamishwa kazi na TFF ya Tanzania.
Image: Facebook

Masaibu yanaendelea kuikumba kambi ya timu ya taifa la Tanzania, Taifa Stars baada ya kuanza vibaya katika kampeni zao za mashindano ya AFCON yanayoendelea nchini Ivory Coast.

Baada ya kocha mkuu Adel Amrouche kutoa matamshi yaliyotajwa kuwa yanalenga kuichafulia jira timu ya taifa ya Morocco kuelekea mechi yao ya ufunguzi, kamati ya nidhamu ya shirikisho la soka barani Afrika, CAF imempiga faini nzito pamoja pia na kumfungia mechi 10 katika bara hili.

Kufuatia matamshi hayo ya uchochezi kwamba Morocco wanapanga matokeo kwa kujichagulia waamuzi katika mechi zao, CAF ilimpata na hatia raia huyo wa Algeria na kumpiga faini ya dola elfu 10 [Ksh 1,617,500].

Ikiwa hiyo haitoshi, shirikisho la soka Tanzania, TFF pia limetoa taarifa kwamba kocha huyo amesimamishwa kazi mara moja na majukumu yake kuchukuliwa na naibu kocha kuiongoza timu katika mechi zilizosalia za AFCON nchini Ivory Coast.

“Shirikisho la mpira wa miguu Afrika, CAF limemfungia mechi nane kocha wa timu ya taifa (Taifa Stars) Adel Amrouche. Adhabu hiyo ilitolewa jana na kamati ya nidhamu ya CAF, malalamiko yaliwasilishwa na shirikisho la mpira wa miguu la Morocco RMFF dhidi ya kocha Amrouche,” taarifa ya TFF ilisoma kwenye ukurasa wao rasmi wa Twitter.

“Katika hatua nyingine, kamati ya utendaji ya shirikisho la mpira wa miguu Tanzania, TFF imemsimamisha kazi kocha Adel Amrouche. Kutokana na uamuzi huo, imemteua Hemed Morocco kuwa kaimu kocha na atasaidiwa na Juma Mgunda,” ilisoma taarifa kwa ukamilifu.

Tanzania kwa sasa wanajiandaa kwa mechi yao ya pili kwenye kundi lao dhidi ya Zambia baada ya kupoteza mechi ya kwanza mikononi mwa Morocco mabao 3-0.