Sadio Mane atuma ujumbe wa kumfariji Mohamed Salah baada ya kupata jeraha AFCON

"Ninamsikitikia kwa sababu kwa bahati mbaya, ni sehemu ya soka," Mane aliwaambia waandishi wa habari baada ya mechi ya Cameroon.

Muhtasari

• “Anataka kuisaidia timu yake na kupata ushindi akiwa na wachezaji wenzake, lakini jeraha liko nje ya uwezo wake.”

Salah na Mane
Salah na Mane
Image: ACE

Winga wa Senegal Sadio Mane ametuma ujumbe wa kumfariji mchezaji mwenzake wa zamani wa Liverpool Mohamed Salah kufuatia jeraha lake dhidi ya Ghana.

Nahodha wa Misri, Mohamed Salah alilazimika kutoka nje akiwa ameumia kwenye kipindi cha mapumziko kwenye sare ya 2-2 ya Mafarao dhidi ya Ghana siku ya Alhamisi.

Uchunguzi huo ulionyesha ni jeraha la msuli wa paja, ambalo litahitaji Salah kukosa michezo miwili pekee, mchezo wa mwisho wa kundi dhidi ya Cape Verde, na hatua ya 16 bora endapo Mafarao watafanikiwa.

Sadio Mane alihakikisha anamuunga mkono Mohamed Salah na kumtakia ahueni ya haraka baada ya kuiongoza nchi yake kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Cameroon na kutinga hatua ya 16 bora.

"Ninamsikitikia kwa sababu kwa bahati mbaya, ni sehemu ya soka," Mane aliwaambia waandishi wa habari baada ya mechi ya Cameroon.

“Anataka kuisaidia timu yake na kupata ushindi akiwa na wachezaji wenzake, lakini jeraha liko nje ya uwezo wake.”

"Ni sehemu ya soka unayopaswa kushughulika nayo, na ninaielewa. Mimi pia nilijeruhiwa kabla ya Kombe la Dunia la 2022, kwa hivyo nina huzuni kwake, lakini hiyo ni soka.”

Bado haijaonekana ni nani atachukua nafasi ya Salah katika michezo hii miwili, huku mastaa kama Ahmed Sayed Zizo, Mahmoud Trezeguet, na Mostafa Fathi wakiwa katika hali ya kusubiri.

Fathi ndiye mchezaji aliyeingia kwa Salah dhidi ya Ghana, lakini kuna uwezekano mkubwa kuwa Zizo ataanza dhidi ya Cape Verde katika nafasi yake ya mrengo wa kulia anayopendelea zaidi.