Olunga asikitika Kenya kuchezea Malawi mechi za nyumbani

Michael Olunga:"Ni hali ya kusikitisha sana kwamba hatuwezi kuchezea hapa nyumbani.."

Muhtasari

•Nahodha wa Kenya amesikitishwa baada ya mechi ya Harambee stars kuwekwa ugani Bingu jijini Lilongwe,Malawi huku akitarajia viwanja vitaimarishwa.

•Kenya itashuka dimbani kumenyana na Burundi mnamo Juni 7,2024 kwenye  mchezo wa kufuzu kombe la dunia 2026.

Michael Olunga. Picha;Facebook
Michael Olunga. Picha;Facebook

Nahodha wa Harambee Stars Michael Olunga ameelezea kusikitishwa kwake na timu ya taifa kushindwa kucheza mechi zao za nyumbani za kufuzu kwa kombe la dunia nchini Kenya.

Kenya italazimika kuwakaribisha Burundi na Ivory Coast nchini Malawi kwa mechi ya kufuzu kwa Kombe la dunia 2026 mwezi ujao kutokana na ukosefu wa uwanja ulioidhinishwa na  FIFA.

Olunga anahisi wachezaji hawatafurahia kuungwa mkono na mashabiki, kwa kuwa hawakucheza nyumbani mara kwa mara katika mechi ya mwisho mwaka jana.

“Ni hasara kubwa kwa sababu unapocheza ugenini, kama tulivyocheza na Gabon, mashabiki wao walikuwa na jukumu kubwa walipokuwa wakiburuza mkia jedwalini, kwa hiyo hii ndiyo aina ya faida ambayo tutaipoteza kwa sababu wakenya wana hamu ya kuiona Harambee Stars ikicheza nyumbani katika mchezo rasmi...'

Aidha Olunga ameitaka serikali kuhakikisha viwanja vinakarabatiwa kwa viwango vya juu ili kuidhinishwa na FIFA.

"Ningependa  tu wizara ya michezo na serikali kuhakikisha kuwepo kwa viwanja vya viwango vya CAF ili  tusirudie makosa yale yale enzi zijazo. Tunataka watu wafurahie timu ya taifa wakiwa nyumbani.”Olunga alisema haya kwenye mahojiano na waandishi wa habari,Ijumaa.

Olunga ametoa matumaini kutokana na ukweli kwamba wachezaji hao watarejea katika uwanja waliouzoea.Kenya inaratibiwa kucheza na Burundi mnamo Ijumaa 7,Juni,2024.

"Tungependa kuwa na mashabiki wetu kwa sababu tumekuwa tukicheza vizuri huko nje lakini ni kwa bahati mbaya hatuwezi kucheza nyumbani lakini siku hizi popote ni nyumbani na wachezaji ni wazuri na watatusukuma."