Modric kusalia Real Madrid kwa mwaka mmoja

"Ninahisi niko nyumbani hapa. Nimesema mara nyingi nataka kustaafu hapa, na ninatumai itafanyika,” Modric alisema.

Muhtasari

•Perez amethibitisha kuwa gwiji wa klabu hiyo, Luka Modric atasalia kwa msimu mwingine baada ya kushuhudia timu yake ikishinda ligi ya mabingwa Ulaya kwa mara ya kumi na tano

•Lucas Vazquez pia alithibitisha kwamba atasalia kwa msimu mwingine,hii ikiwa ni taarifa njema kwa miamba hao wa Uhispania.

Luka Modric
Image: Getty Images

Rais wa Real Madrid, Florentino Perez amethibitisha kuwa gwiji wa klabu hiyo, Luka Modric atasalia kwa msimu mwingine baada ya kushuhudia timu yake ikishinda ligi ya mabingwa Ulaya kwa mara ya kumi na tano

Hii inakuja baada ya miezi kadhaa ya uvumi kuhusu hatma ya mchezaji huyo, ambayo sasa imethibitishwa  ni kusalia Real Madrid kwa mwaka mwingine.

"Luka Modric hakika ataendelea na sisi kwa msimu mwingine...Hakuna shaka juu ya hilo. Tuna furaha sana kuwa naye,yeye ni mmoja wa magwiji wakubwa wa klabu hii." Perez alidokoa.

"Real Madrid ndiyo klabu ya maisha yangu. Ninahisi niko nyumbani hapa. Nimesema mara nyingi nataka kustaafu hapa, na ninatumai itafanyika,” Modric alisema.

Modric aliingizwa uwanjani dakika ya 85 wakati timu yake iliposhinda fainali ya ligi ya mabingwa dhidi ya Borussia Dortmund Jumamosi, huku timu yake ikiwa mbele kwa 2-0. Ushindi huo unamaanisha kuwa sasa ameandikisha ushindi mara sita katika michuano hiyo, na kuongeza idadi kubwa ya medali za fedha za kifahari.

Lucas Vazquez pia alithibitisha kwamba atasalia kwa msimu mwingine,hii ikiwa ni taarifa njema kwa miamba hao wa Uhispania.

 "Inaonekana nitakaa kwa mwaka mwingine." Vazquez alisema.

Kwa sasa inabakia kuonekana kile ambacho Nacho ataamua kufanya kwa mustakabali wake baada ya kandarasi yake kukamilika lakini ni ishara nzuri kwa Real Madrid kuwa Modric na Vazquez watasalia.