Firat ana imani na kikosi cha Harambee Stars

Kocha mkuu wa Harambee Stars,Engin Firat ameelezea imani ya kutwaa ushindi dhidi ya Burundi na Cote d'Ivoire kwenye mechi za kufuzu kombe la dunia,2026 kule Malawi.

Muhtasari

•Firat ameelezea imani na wachezaji wake hasa baada ya mazoezi ya wiki jana ugani Police Sacco jijini Nairobi.

•Harambee stars wapo jijini Lilongwe,Malawi kwa matayarisho kwa ajili ya mechi dhidi ya Burundi Ijumaa 7,Juni 2024.

Kocha wa Harambee Stars
Kocha wa Harambee Stars
Image: Facebook

Kocha mkuu wa Harambee Stars Engin Firat ameelezea matumaini yake kuhusu maandalizi ya timu yake kwa mechi za kufuzu kwa kombe la dunia 2026.

Timu hiyo iliyowasili Lilongwe, Malawi siku ya Jumapili, imekuwa ikijiandaa kwa mechi mbili muhimu. Kenya itamenyana na  Burundi Juni 7 kabla ya kukutana na mabingwa wa Afrika Cote d'Ivoire mnamo Juni 11.

 Akiongea na waandishi wa habari,Firat amefurahishwa na maendeleo ya timu hiyo wakati wa kambi yao ya wiki moja katika uwanja wa Police Sacco jijini Nairobi.

"Tumejiandaa vyema kwa kazi iliyo mbele yetu na tunaweza kufikia lengo letu kwa umakini na juhudi," Firat alisema.

Firat ana imani kuwa uzoefu katika uwanja wa kitaifa wa Bingu, ambapo Kenya ilishinda michuano ya mwaliko ya mataifa manne mwezi Machi kwa kuwalaza Malawi 4-0 na Zimbabwe 3-1, kutawawezesha kuwapa motisha.

"Habari njema ni kwamba hivi majuzi tulicheza hapa miezi michache iliyopita na tunafahamu mambo ya ndani. Hilo linaweza kutupa motisha zaidi." Firat aliongeza.

Aidha,Firat alikariri umuhimu wa kupata pointi nyingi zaidi katika mechi hizi ili kuimarisha nafasi yao ya kufuzu moja kwa moja.

"Tuko hapa kuchagua ushindi muhimu. Tunahitaji pointi nyingi zaidi ili kuimarisha nafasi yetu ya kufuzu moja kwa moja kwa kombe la dunia."

Kenya iko katika nafasi ya tatu katika Kundi 'F' nyuma ya Cote d'Ivoire na Gabon. Wengine katika kundi hilo ni Ushelisheli, ambao Kenya waliwazaba mabao 5-0 katika mechi yao ya mwisho mjini Abidjan.

Timu moja pekee katika kundi hilo itafuzu kwa kombe la dunia la timu 48, ambalo litachezwa katika miji 16 ya Canada, Mexico na Amerika. Washindi wanne kati ya washindi wa pili bora kutoka kwa makundi tisa watapata nafasi katika mchujo ambao utaamua mwakilishi wa CAF katika mchujo wa mashirikisho baina ya mashirikisho yanayohusisha timu sita kuamua nafasi mbili za mwisho za kombe la dunia.