Maelezo ya mkataba mpya wa Kylian Mbappe na Real Madrid

Real Madrid wametangaza rasmi usajili wa mshambuliaji mahiri wa Ufaransa, Kylian Mbappe.

Muhtasari

•Real Madrid ilitoa taarifa Jumatatu jioni ikifichua kuwa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 amesaini mkataba wa miaka mitano.

•Mchezaji huyo wa miaka 25 alisema ni "ndoto iliyotimia" kuhusu uhamisho wake wa muda mrefu wa kwenda Real Madrid.

wametangaza usajili wa mshambuliaji Kylian Mbappe.
Real Madrid wametangaza usajili wa mshambuliaji Kylian Mbappe.
Image: HISANI

Miamba wa soka wa Uhispania Real Madrid wametangaza rasmi usajili wa mshambuliaji mahiri wa Ufaransa, Kylian Mbappe.

Real Madrid ilitoa taarifa Jumatatu jioni ikifichua kuwa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 amesaini mkataba wa miaka mitano.

"Real Madrid C.F na Kylian Mbappe wamefikia makubaliano ambapo atakuwa mchezaji wa Real Madrid kwa misimu mitano ijayo," klabu hiyo ilisema katika taarifa.

Nahodha huyo wa timu ya taifa ya Ufaransa amejiunga na miamba hao wa soka nchini Uhispania kwa uhamisho wa bila malipo kufuatia kuisha kwa mkataba wake katika Paris Saint-Germain. Mbappe amekuwa akichezea mabingwa hao wa Ligue 1 katika miaka kadhaa iliyopita tangu 2017.

Akizungumza baada ya uhamisho huo, mchezaji huyo wa miaka 25 alisema ni "ndoto iliyotimia" kuhusu uhamisho wake wa muda mrefu wa kwenda Real Madrid.

"Hakuna anayeweza kuelewa jinsi nilivyofurahi kwa sasa! Ndoto imetimia. Nina furaha na kujivunia kujiunga na klabu ya ndoto zangu," Mbappe alisema.

Duru za kuaminika zinasema kuwa atapokea mshahara wa euro 15m (£12.8m) kwa msimu, pamoja na bonasi ya kusajili ya euro 150m (£128m) kwa miaka mitano, na atahifadhi asilimia ya haki zake za picha.

Mbappe anajiunga na timu ya Madrid baada tu ya kushinda La Liga na Ligi ya Mabingwa. Real ilishinda Kombe lao la 15 la bara Uropa kwa ushindi dhidi ya Borussia Dortmund katika fainali ya Ligi ya Mabingwa siku ya Jumamosi.