Kocha wa Ubelgiji awashinikiza wachezaji wake kujiamini kwenye mechi dhidi ya Ufaransa

Belgium itavaana na Ufaransa katika mechi ya hatua ya kumi na sita bora kwenye mashindano ya Euro 2024 saa moja jioni

Muhtasari

•Kocha mkuu wa Ubelgiji,Domenico Tedesco amesema kuwa sharti wachezaji wake wawe na ujasiri tosha kabla ya mechi dhidi ya Ufaransa.

•Ufaransa wameshinda mechi zao zote nne za awali dhidi ya Ubelgiji kwenye michuano mikubwa (Kombe la Dunia na Euro), wakifunga mabao 13 na kuruhusu matatu pekee.

kocha mkuu wa Ubelgiji
Domenico Tedesco kocha mkuu wa Ubelgiji
Image: Ghetty images

Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Ubelgiji Domenico Tedesco amesema kuwa ni sharti timu yake iwe na imani   kabla ya pambano la leo dhidi ya Ufaransa ili kufuzu kwa hatua ifuatayo ya mashindano ya Euro 2024.

Wachezaji wa Ubelgiji huenda walipoteza imani kutokana na chuki ya mashabiki wao katika sare ya 0-0 dhidi ya Ukraine, ambayo iliiwezesha Ubelgiji kusonga mbele lakini si kama washindi wa kundi, na si kwa kiwango kilichotarajiwa.

Ubelgiji wanachuana na timu ya Ufaransa ambayo pia haijafanya vizuri na kumaliza nafasi ya pili kwenye kundi lao nyuma ya Austria.

Kwenye mazungumzo na wanahabari,Tedesco amesema kuwa sharti wachezaji wake  wawe na ujasiri mkubwa kabla ya mechi ya leo.

"Tulifanyia kazi imani hii siku mbili au tatu zilizopita, kwa sababu kama hakuna imani, hakuna kitu. Kwa hiyo inabidi tuamini na kila mtu anajua kwamba tunahitaji mchezo wa hali ya juu kabisa."Tedesco alisema.

Ubelgiji walimaliza wa pili kwenye Kundi E nyuma ya Romania, na walifunga mabao mawili pekee katika michezo yao mitatu ya kundi, huku Ufaransa nao wakifunga mabao mawili pekee,moja likiwa ni   bao la kujifunga kutoka kwa wapinzani  na lingine likiwa ni penalti.

Hii itakuwa mechi ya 76 ya Ufaransa na Ubelgiji. Ubelgiji ndio wapinzani wa muda wote wa Ufaransa, wamekutana nao karibu mara mbili ya timu nyingine yoyote.

Timu itakayoshinda kwenye mechi ya leo ,Julai 1 itamenyana na  mshindi kati ya Ureno na Slovenia kwenye hatua ya robo fainali.