Arsenal hatimaye yamsajili rasmi kipa David Raya kutoka Brentford

Kipa wa Uhispania David Raya ametia saini mkataba wa kudumu na Arsenal.

Muhtasari

•Arsenal ilitangaza kumsaini Raya Alhamisi jioni kupitia majukwaa yake ya mtandaoni ikifichua kuwa ametia saini kandarasi ya muda mrefu.

•Klabu hiyo iliendelea kuzungumzia jinsi mlinda mlango huyo wa Uhispania alikuwa sehemu muhimu ya mafanikio ya msimu uliopita.

Image: TWITTER// ARSENAL

Kipa wa Uhispania David Raya ametia saini mkataba wa kudumu na Arsenal, baada ya msimu wa 2023/24 kwa mkopo wenye mafanikio makubwa katika klabu hiyo.

Klabu hiyo yenye maskani yake Kaskazini mwa London ilitangaza kumsaini Raya siku ya Alhamisi jioni kupitia majukwaa yake rasmi ya mtandaoni ikifichua kuwa ametia saini kandarasi ya muda mrefu.

Kipa huyo mwenye umri wa miaka 28 alikaa msimu mzima wa 2023/24 katika Emirates baada ya kusajiliwa kwa mkopo kutoka klabu nyingine ya EPL, Brentford.

"David Raya ametia saini mkataba wa muda mrefu na klabu kukamilisha uhamisho wake wa kudumu kutoka Brentford," Arsenal ilitangaza kupitia tovuti yake rasmi.

Klabu hiyo iliendelea kuzungumzia jinsi mlinda mlango huyo wa Uhispania alikuwa sehemu muhimu ya mafanikio ya msimu uliopita.

“Kipa huyo mwenye umri wa miaka 28 alikaa nasi msimu uliopita kwa mkopo na ilikuwa sehemu muhimu ya mafanikio tuliyofurahia na historia tuliyoweka. Alicheza mechi 41 katika mashindano yote, huku akiweka pasi 20 safi. Kumi na sita kati ya mechi hizo zilikuwa kwenye Ligi ya Premia na walimpa David tuzo ya Golden Glove ya Ligi Kuu ya 2023/24,” walisema.

Kabla ya kujiunga na Wanabunduki kwa mkopo msimu uliopita, mlinda mlango huyo mwenye umri wa miaka 28 alikuwa ameiwakilisha Brentford kwa takriban miaka minne tangu 2019 ambapo alihusika katika michezo 161.

Alishinda glovu ya dhahabu katika msimu wa EPL 2023/24 baada ya kutoruhusu bao katika michuano 20 kati ya mechi 41 alizoichezea Arsenal.