Gabriel Jesus atoa taarifa baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti

Mshambulizi huyo alithibitisha kuwa ameruhusiwa kuenda nyumbani baada ya upasuaji.

Muhtasari

•Kufuatia jeraha hilo, mchezaji huyo wa timu ya taifa ya Brazil alisafiri hadi London ambako alifanyiwa upasuaji wa goti. 

•Pichani, alikuwa na plasta kwenye mguu wake wa kulia ambao ulifanyiwa upasuaji kufuatia jeraha alilopata.

Mshambulizi wa Brazil na Arsenal, Gabriel Jesus
Image: TWITTER// GABRIEL JESUS

Mshambulii wa Arsenal Gabriel Jesus anaendelea kupata afueni nyumbani baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti siku ya Jumanne.

Jesus alilazimika kutoka kwenye mashindano ya Kombe la Dunia yanayoendelea nchini Qatar baada ya kupata jeraha mbaya la goti wakati wa mechi ya Brazil dhidi ya Cameroon siku ya Ijumaa wiki iliyopita.

Kufuatia jeraha hilo, mchezaji huyo wa timu ya taifa ya Brazil alisafiri hadi London ambako alifanyiwa upasuaji wa goti. 

"Gabby sasa ataanza mpango wake wa matibabu. Kila mtu katika klabu anamuunga mkono Gabby na tufanya kazi kwa bidii kumrudisha uwanjani haraka iwezekanavyo," Klabu ya Arsenal  ilisema katika taarifa.

Siku ya Jumatano, mshambulizi huyo alitoa taarifa na kuthibitisha kuwa ameruhusiwa kuenda nyumbani baada ya upasuaji.

"Ni wakati wa kuenda nyumbani," alisema kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii.

Jesus aliambatanisha ujumbe huo na picha za video ziilizomuonyesha akitembea kwa usaidizi wa mikongojo.  Pichani, alikuwa na plasta kwenye mguu wake wa kulia ambao ulifanyiwa upasuaji kufuatia jeraha alilopata.

Image: TWITTER// GABRIEL JESUS

Katika video nyingine ambayo alichapisha siku ya Alhamisi, mshambulizi huyo alionekana akiwa ametulia nyumbani na binti yake.

Baada ya kupata jeraha, Jesus alitoa taarifa akiwashukuru watu ambao walichukua hatua ya kumfariji kwa jumbe.

"Ikiwa kuna ratiba na ningeweza kukuona na kukuambia kitu, ningesema "Gabriel, wewe ni mshindi". Asante kwa kila mtu ambaye alituma ujumbe wa msaada na upendo. 🙌🏾🙏🏾," aliandika chini ya picha yake akiwa mtoto.

Klabu ya Arsenal ambayo inaoongoza kwenye jedwali la EPL sasa inatarajiwa kukosa huduma za Jesus kwa takriban miezi mitatu. Kufuatia hilo, shinikizo limeendelea kuongezeka kwa kocha Mikel Arteta kusajili mshambulizi mpya