Sofiane Boufal wa Morocco aomba radhi kwa kutotambua Afrika kufuatia ushindi wao

Boufal alisema ushindi huo wao mkubwa ni wa Morocco, Waislamu na Waarabu.

Muhtasari

•"Shukrani kwa Wamorocco wote duniani kote kwa uungaji mkono wao, kwa Waarabu wote, na Waislamu wote," Boufal alisema.

•Siku ya Jumatano, mchezaji huyo wa Angers SCO aliwaomba radhi Waafrika wote kwa kusahau bara Afrika.

Mchezaji wa Morocco Sofiane Boufal
Image: HISANI

Mshambulizi wa  timu ya taifa ya Morocco Sofiane Boufal alizua gumzo kubwa kwenye mitandao ya kijamii baada ya kutotambua bara Afrika wakati akisherehekea kufuatia ushindi wao dhidi ya Uhispania siku ya Jumanne.

Morocco iliingia kwenye rekodi kama nchi ya nne ya Afrika kufuzu kwa robo fainali ya Kombe la Dunia baada ya kuishinda Uhispania 3-0 katika mikwaju ya penalti.

Mchuano wa kusisimua kati ya Morocco na mabingwa hao wa Kombe la Dunia mwaka wa 2010 haukuwa na bao lolote katika muda wa kawaida na muda wa ziada na hivyo ikabidi kuamuliwa kwa mikwaju ya penalti. Kiungo wa kati wa Sampdoria Abdelhamid Sabiri, Hakim Ziyech wa Chelsea na Beki wa kulia wa PSG Achraf Hakimi walifunga penalti tatu za Morocco huku Uhispania ikishindwa kufunga penalti yoyote kati ya tatu walizopiga.

Wakati akizungumza na vyombo vya habari, Boufal alisema ushindi huo wao mkubwa ni wa Morocco, Waislamu na Waarabu.

"Shukrani kwa Wamorocco wote duniani kote kwa uungaji mkono wao, kwa Waarabu wote, na Waislamu wote," alisema.

Matamshi yake yalizua ghadhabu kubwa haswa miongoni mwa Waafrika ambao waliipigia upato Morocco kufuzu kwa robo fainali.

Asilimia kubwa ya Waafrika ambao walienda nyuma ya Morocco baada ya kubanduliwa kwa Senegal, Ghana, Tunisia na Cameroon  walivunjwa moyo baada ya Boufal kukosa kuwashukuru kwa sapoti yao.

Siku ya Jumatano, mchezaji huyo wa Angers SCO aliwaomba radhi Waafrika wote kwa kusahau bara Afrika.

"Samahani kwa kusahau kutaja Bara lote la Afrika jana kwenye mahojiano ya baada ya mechi. Asanteni kwa kuwa nyuma yetu, pia natoa ushindi kwenu bila shaka. Tunajivunia kuwawakilisha ndugu zetu wote  katika bara. PAMOJA ... " alisema kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Morocco sasa itamenyana na Ureno katika hatua ya raundi ya robo fainali mnamo Jumamosi, Desemba 10.