Mzee aliyenaswa na kamera akimsihi shabiki mrembo ampe namba aomba msamaha kwa mkewe

Shabiki huyo wa Ivory Coast amewaomba radhi mkewe, familia yake na mwanadada aliyejaribu kutongoza.

Muhtasari

•Shabiki huyo alinaswa akijaribu kumtongoza mwanadada mdogo mwenye sura nzuri wakati wa mechi kati ya wenyeji na Senegal.

•Santos alisimulia alivyomuona shabiki huyo mrembo wa Senegal na kumwendea kuomba namba yake kabla hajamdharau waziwazi.

alirekodiwa akiomba namba ya shabiki wa kike
Anselme Santos alirekodiwa akiomba namba ya shabiki wa kike
Image: HISANI

Shabiki wa Ivory Coast ambaye alinaswa na kamera akijaribu kumtongoza mwanadada mdogo mwenye sura nzuri wakati wa mechi ya hatua ya 16 bora ya Kombe la Mataifa ya Afrika kati ya wenyeji na Senegal amevunja ukimya kuhusu kile kilichotokea.

Video ya Bw Anselme Santos ilisambaa kwenye mitandao ya kijamii mapema wiki hii huku wanamitandao wakitoa hisia mseto kuhusu kile kilichoonekana. Alionekana akijaribu kupata usikivu wa mwanadada huyo mrembo ambaye alionyesha kutopendezwa naye, na kupelekea kejeli na ukosoaji mkubwa kutoka kwa wanamitandao. Baadhi ya watumiaji wa mtandao hata walipendekeza kuwa Bw Santos alikuwa Sugar Daddy wa msichana huyo.

Kufuatia hayo, Bw Santos Jumatano alialikwa kwenye kipindi cha mtangazaji Willy Dumbo ambapo alifichua ukweli kuhusu kisa hicho kizima ambacho kilizua mjadala kwenye mitandao ya kijamii.

“Mashabiki wote wa Ivory Coast walikuwa na furaha siku hiyo, kwa sababu tulikuwa na timu imara sana. Kutoka hotelini, tulikuwa tukichezea Wasenegali. Tulipanda basi pamoja ili kufika uwanjani. Mara baada ya hapo, Ivory Coast ilifungwa bao la kwanza, jambo ambalo lilituhuzunisha. Wasenegali walikuwa wakijaribu kututania, lakini huo ndio mchezo,” Bw Santos alisimulia.

Aliendelea kusimulia jinsi alivyomuona shabiki huyo mrembo wa Senegal na kumwendea kuomba namba yake kabla hajamdharau waziwazi.

 “Wakati Ivory Coast iliposhinda, mimi pia nilianza kuwatania Wasenegali. Nilikuwa nimeketi juu. Nilipomwona yule mwanadada akipeperusha bendera ya Senegal, nilimwendea ili kumpa changamoto. Tulikuwa tukiburudika. Katika furaha hiyo, nilimwambia: ‘Nipe namba yako, nipe namba yako’. Haikuwa mbaya, lakini hakutaka. Kwa hivyo sikusisitiza. Hata baadaye, sikuileta tena. Nilirudi stendi,” alisimulia.

Kufuatia athari za video hiyo iliyosambaa, shabiki huyo wa Ivory Coast alichukua fursa hiyo kuomba msamaha kutoka kwa mkewe na familia yake kwa ujumla.

“Napenda kuchukua nafasi hii kumwomba radhi mwanadada huyo, kwa wote walio karibu naye, kwa mke wangu na watoto wangu. Sikuwahi kufikiria kuwa video hii ingeenea kote ulimwenguni,” Enselme Santos alisema.

Bw Santos alikuwa miongoni mwa maelfu ya mashabiki walioshuhudia Ivory Coast ikipata ushindi wa kustaajabisha dhidi ya mabingwa watetezi Senegal mnamo Januari 29 katika Uwanja wa Charles Konan Banny mjini Yamoussoukro.