Pigo kwa Arsenal huku Gabriel Jesus akilazimika kufanyiwa upasuaji, kuwa nje wiki kadhaa

Arteta alitangaza kuwa mshambuliaji huyo hataweza kucheza kwa wiki kadhaa huku akiendelea kupata nafuu.

Muhtasari

•Mikel Arteta alithibitisha kwamba Mbrazil huyo alifanyiwa upasuaji mdogo Jumatano asubuhi baada ya kusumbuliwa na goti .

•Arteta alifichua kuwa jeraha la mshambuliaji huyo linahusiana na jeraha la awali alilopata wakati Kombe la Dunia.

Image: INSTAGRAM// GABRIEL JESUS

Klabu ya soka ya Arsenal itakosa huduma za mshambuliaji matata Gabriel Jesus kwa muda wa wiki zisizojulikana huku Ligi Kuu ya Uingereza ikitarajiwa kuanza katika kipindi kisichozidi siku 10.

Siku ya Jumatano jioni, mkufunzi wa Arsenal, Mikel Arteta alithibitisha kwamba Mbrazil huyo mwenye umri wa miaka 26 alifanyiwa upasuaji mdogo mnamo Jumatano asubuhi baada ya kusumbuliwa na goti mara kwa mara.

Arteta alitangaza kuwa mshambuliaji huyo hataweza kucheza kwa wiki kadhaa huku akiendelea kupata nafuu kutokana na utaratibu huo.

“Kwa bahati mbaya alifanyiwa upasuaji kidogo asubuhi ya leo. Alikuwa na usumbufu katika goti lake ambao umekuwa ukisababisha mashida kadhaa, na ilibidi wamchunguze na kuyasuluhisha. Sio upasuaji mkubwa lakini atakuwa nje kwa wiki chache nadhani,” Arteta aliambia wanahabari baada ya mechi ya Kombe la Emirate dhidi ya Monaco Jumatano jioni.

Mhispania huyo alibainisha kuwa ni pigo kubwa kuona Jesus akilazimika kufanyiwa upasuaji huo na kudokeza kwamba mchezaji huyo wa Kimataifa wa Brazil alikuwa ameanza kurejea katika hali yake nzuri kabla ya kupata usumbufu kwenye goti lake.

"Alikuwa katika hali nzuri lakini tumempoteza. Amekuwa akihisi usumbufu katika wiki chache zilizopita na ilibidi waangalie na tulilazimika kufanya uamuzi na bora zaidi ni kumlinda mchezaji na kumrudisha haraka iwezekanavyo. Tuliamua kufanya hivyo,” alisema.

Arteta alifichua kuwa jeraha la mshambuliaji huyo linahusiana na jeraha la awali alilopata wakati Kombe la Dunia akiwa na taifa lake Brazil mwishoni mwa mwaka jana.

Mwezi Desemba mwaka jana, Jesus alifanyiwa upasuaji wa goti baada ya kuumia alipokuwa akiichezea Brazil katika michuano ya Kombe la Dunia la Fifa iliyofanyika nchini Qatar. Mshambulizi huyo mwenye umri wa miaka 26 alikosa sehemu kubwa ya awamu ya pili ya msimu wa 2022/23, jambo ambalo lilikuwa pigo kubwa kwa Arsenal ambao walimtegemea sana kufunga mabao.

Kwa bahati nzuri aliweza kumaliza msimu vizuri nao na hata ameshiriki katika mechi kadhaa za kujiandaa na msimu kabla ya kufanyiwa utaratibu mdogo Jumatano asubuhi.