Richarlison achorwa tattoo ya kushangaza baada ya Brazil kubanduliwa nje ya Kombe la Dunia

Tattoo hiyo inaonekana kuwa njia ya kujisherehekea yeye, Neymar na Ronaldo.

Muhtasari

•Richarlson alichorwa tattoo hiyo siku chache zilizopita baada ya timu ya Brazil kubanduliwa nje ya Kombe la Dunia.

•Brazil ilibanduliwa nje ya Kombe la Dunia wiki jana baada ya kupoteza mechi ya robo fainali dhidi ya Croatia.

Richarlison na Gwiji wa Brazil Ronaldo De Lima
Image: INSTAGRAM// RICHARLSON

Mchezaji wa timu ya taifa ya Brazil, Richarlison de Andrade amewashangaza wengi baada ya kuchorwa tattoo kubwa ya yeye, mchezaji mwenzake Neymar na gwiji wa Brazil Ronaldo de Lima kwenye mgongo wake.

Richarlison alichorwa tattoo hiyo siku chache zilizopita baada ya timu ya Brazil kubanduliwa nje ya Kombe la Dunia.

Brazil ilibanduliwa nje ya mashindano ya Kombe la Dunia wiki jana baada ya kupoteza mechi ya robo fainali dhidi ya Croatia.  Mshindi wa mechi hiyo aliamuliwa kwa matuta ya penalti baada ya kuisha sare ya 1-1.

Ilikuwa imeonekana kana kwamba Neymar ameishindia Brazil baada ya kufunga bao zuri la pekee katika muda wa nyongeza  lakini Bruno Petković alivunja mioyo yao kwa bao la dakika za mwisho na kusawazisha.

Kipa wa Croatia Dominik Livaković aliibuka shujaa katika hatua ya penalti, akiokoa juhudi ya kwanza ya Rodrygo kabla ya beki Marquinhos kuona mkwanju wake ukigonga nguzo, kupeleka Croatia hadi nusu fainali.

Kupoteza kwa Brazil kulivunja mioyo sio tu ya Wabrazil bali pia ya mashabiki wengi kote duniani ambao walikuwa wamepigia upato timu hiyo kushinda Kombe la Dunia la mwaka huu. Croatia ambao waliwabandua nje Brazil waliendelea kutimuliwa na timu ya Argentina katika hatua ya nusu fainali.

Ni baadaye ambapo Richarlison aliadhimisha safari yake ya Kombe la Dunia na timu ya Brazil kwa kupata tattoo mpya mgongoni. Tattoo hiyo inaonekana kuwa njia ya kujisherehekea yeye mwenyewe, Neymar na Ronaldo.


Tattoo ya Richarlison
Image: HISANI

Richarlison alifunga mabao mawili, ikiwa ni pamoja na bao la sarakasi (bicycle kick), na kuisaidia timu ya Brazil kuanza kampeni ya Kombe la Dunia la FIFA 2022 kwa ushindi wa 2-0 dhidi ya Serbia.

Alifunga bao lingine la kipekee katika ushindi wao dhidi ya Korea Kusini katika hatua ya mwondoano.