Spika Lusaka hupokea simu kabla ya kufanya uamuzi- Murkomen

Aliyekuwa kiongozi wa wengi bungeni seneti Kipchumba Murkomen amemtaka Spika Ken Lusaka kujiuzulu.

Akiongea Jumatatu kwenye mahojiano na Redio Citizen, Murkomen alisema Lusaka ameshindwa kutetea uhuru wa seneti na kwa hivyo anafaa kujiondoa.

"Sasa Lusaka unajua ameshindwa kusimamia seneti na anafaa ajiondoe ili tupate Spika mwingine ambaye ataweza kusimamia uhuru wa seneti kama tuliyekuwa naye Spika Ethure," Murkomen alisema.

Seneta huyo alisema shida ya Lusaka ni kuwa anapata presha kutoka kwa vigogo wa kisiasa na hivyo uamuzi wake kwa masuala ya seneta huwa si huru.

"Ameshindwa kabisa kupigania uhuru wa seneti, akipigiwa simu moja anatetemeka sana," aliongeza seneta huyo.

Murkomen alisema ukosefu wa uhuru wa bunge la seneti utawekwa wazi wakati wa kuskizwa kwa mashtaka dhidi ya Gavana Anne Waiguru yaliyoletwa na MCAs wa kaunti ya Kirinyaga.

"Mimi nataka niwaambie wakazi wa Kirinyaga pole sana, wengine wetu tutajaribu lakini hatma itaamuliwa na Raila Odinga na viongozi wengine ndani ya Jubilee," Murkomen aliongeza.

Hoja kuhusu jinsi kesi ya kutimuliwa kwa Waiguru itakuwa kwenye seneti Jumanne, Juni 16.