Valentine’s Day – Siku moja yenye makovu na kumbukumbu ambazo baadhi ya watu hutaka kusahau

red-rose-image-6
red-rose-image-6

Na Yusuf Juma

Tarehe 14 Februari kila mwaka huwa siku ya kipekee kwa wanaoamini kuhusu huba. Wapenzi na wanaogiza kupendana huitumia siku hii kudhihirisha wazi na pia kuwapa ‘surprises’ wapendwa wao. Lakini chini ya kivuli cha siku hii, kuna visa vya makovu yanayoambatana na machozi kwa baadhi yetu. Haya ni baadhi ya masimulizi ya masaibu yaliyowapata wachache ambao waliamini sana kuhusu penzi lakini siku ya valentines ilifika kwa kishindo na kuwavunja nyoyo. Wengine hadi sasa hawajawahi kupona nyoyo au kuchukua hatua nyingine kuhusu masuala ya mahusiano. Wengine waliapa kwamba katu hawatompenda mtu wa asilimia 100.

‘Break up’

Jared Onchori anaikumbuka kila siku ya valentine kama maadhimisho ya Februari katili ya mwaka 2012 alipotengana na mchumbake wa miaka mitatu. Katika chuo kimoja kikuu hapa jijini, Jared na Phylis walikuwa mfano kwa wenzao –kuhusu jinsi mapenzi kamili yanavyofaa kuwa. Wengi waliowaonea kijicho lakini wengi zaidi walitaka kuwa wao. Sio darasani, sio kwenye maktaba – Jared na Phylis walikuwa pamoja ‘Always’. Januari na makali yake mwaka huo ilipotamatika, Jared katika fikra zake alikuwa amepanga na kurejeleza ndotoni kila hatua ya kumbwagia mchumbake Phylis ‘proposal’ ya ndoa. Alikuwa na uhakika unaojaa miaka yote alioishi kwamba Phylis angekuwa mke wake. Lakini maisha yana ukatili! siku ya valentine mwaka wa 2012, Jared aligundua kwamba Phylis alikuwa na mchumba mwingine. Mchumba huyo mwingine alikuja chuoni na kila aina ya zawadi na mbwe mbwe ili kumtoa pumzi Phylis. Usiku huo Phylis hakurejea chuoni na ndio iliyokuwa siku ya mwisho ya uhusiano wake na Jared.

Usaliti

Ni jambo la kufadhaisha kugundua kwamba mumeo au mkeo ana asali ya nje. Lakini kwa Natasha, machungu ya kugundua hilo yalikuja kwa ‘Double dose’ kwani pia katika siku ya valentine mwaka wa 2015, aling’amua kwamba mumewe wa miaka minne alikuwa pia akila uroda na dadake! Natasha alikuwa akiishi na dadake mdogo aliyemaliza kidato cha nne akingoja kujiunga na chuo cha anuwai. Lakini nyuma ya tabasamu alizoziona kati ya mumewe na dadake , kulikuwa na jungu kubwa la usaliti. Walikuwa wakionana kimwili kisiri lakini hakuna aliyegundua uharamu huo. Wongo ulichoka kujificha siku ya valentine 2015 wakati Natasha alipopata Bunda la maua ya gharama ya juu. Chupa nzito ya Kileo ghali na kijikaratasi chenye ujumbe mfupi wa mapenzi ambao mumewe alimwandikia dadake Natasha. Kisirani kiliwapata wawili hao wakati aliyetumwa kuzipeleka zawadi hizo alipokosa kuwatofautisha mtu na dadake! Natasha , kamwe hajasahau usaliti huo na valentine’s day, inamletea kumbukumbu hizo.

Missing in Action

Esther* Hakumbuki wakati wa mwisho ambapo siku ya valentine ilimpata pamoja na mumewe. Kila wakati wa valentine , mumewe ambaye ni mfanyibiashara hupatwa na shughuli ya dharura na husafiri kwa ghafla. Halalamiki kwamba lazima wawe pamoja lakini anashangaa mbona safari hizi hutokea siku moja kabla ya valentine au katika siku hiy. Ingawaje amekuwa akitumiwa zawadi na mumewe katika siku zote za valentines, Esther ana kinyongo kuhusu kutokuwepo kwake na anashuku huenda kuna mtu ambaye huchuma alikopanda yeye.

Ni bayana kwamba visa ni vingi vya wasiotaka kulisikia jina la valentine’s lakini huko nje, najua kuna wengi ambao siku hii humaanisha zaidi ya zawadi. Kuwepo na kuwakumbusha wapendwa wetu tunavyowajali ni mojawapo ya njia bora za kuadhimisha siku ya wapendanao. Ujumbe mfupi, hata wa emoji ..unaweza kumpa mtu tabasamu ajue kwamba kuna anayemjali. Kwenu nyote mlio na upendo na mnaopendana ..Go Paint the town Red!