"Tafadhali usiropokwe" Gidi atuma ujumbe muhimu kwa DP Gachagua kabla ya ziara ya Jill Biden

Gidi alimuomba naibu rais 'asichome picha' wakati akimlaki mgeni huyo maalum.

Muhtasari

•Jill anatarajiwa kufanya ziara yake ya kwanza nchini Kenya tangu mumewe achaguliwe kuwa Rais wa Marekani.

•"Kwa mfano ukienda kumpokea pale kwa airport. Tafadhali bwana Riggy G naomba usimwambie Jill Biden, 'Hey, umelost!" Gidi alimwabia DP.

Mtangazaji Gidi Ogidi na naibu rais Rigathi Gachagua

Mtangazaji wa kipindi cha Gidi na Ghost asubuhi kwenye Radio Jambo, Gidi Ogidi Gidi amemsihi naibu rais Rigathi Gachagua kudumisha utulivu wake wakati mke wa rais wa Marekani Jill Biden atatembelea Kenya siku ya Ijumaa.

Jill anatarajiwa kufanya ziara yake ya kwanza nchini Kenya tangu mumewe, Joe Biden, achaguliwe kuwa Rais wa Marekani na atakaribishwa na viongozi wakuu wa serikali akiwemo mke wa rais wa Kenya, Rachel Ruto.

Wakati wa shoo ya Ijumaa asubuhi, Gidi kwa utani alimuomba naibu rais 'asichome picha' wakati akimlaki mgeni huyo maalum.

"Riggy G. Tuko na mgeni. Tafadhali tafadhali tafadhali usiropokwe leo," Gidi alisema.

Aliendelea, "Kwa mfano ukienda kumpokea pale kwa airport. Tafadhali bwana Riggy G naomba usimwambie Jill Biden, 'Hey, umelost!"

Mtangazaji huyo mahiri alibainisha kuwa DP Rigathi Gachagua anapenda kutumia msemo huo sana. Hata hivyo, alidokeza kuwa unaweza kumfanya Jill Biden ashangae ni nini kinaendelea ilhali tayari atakuwa nchini.

Jill Biden alitangaza ziara ya Afrika mapema wiki hii na akabainisha kuwa ni mara yake ya kwanza kama mke wa rais.

Kabla ya kuja Kenya, kwanza alizuru Namibia ambako alishiriki katika harakati za vijana katika nchi hiyo anayoamini ina demokrasia imara.

Nchini Kenya, Jill Biden atakutana na kushirikiana na wale walioathiriwa na ukame na wanaokabiliwa na uhaba wa chakula.

"Kisha nchini Kenya, nitasikia kutoka kwa wale walioathiriwa na ukame wa kihistoria unaoendelea na uhaba wa chakula, ambao umechochewa na athari mbaya za shambulio la Urusi kwa Ukraine," alisema.

Mkewe huyo wa Rais wa Marekani alisema licha ya kuwa Kenya iko maili mbali na Marekani, chochote kinachoathiri taifa pia kinawaathiri huko ng'ambo.

"Ulimwengu wetu umeunganishwa. Kinachotokea baharini, kinatuathiri sisi sote," Jill alisema.

Jill alisisitiza kwamba amekuwa na usaidizi mkubwa kwa wanawake na vijana ulimwenguni kote.

"Siku zote nimekuwa nikiamini kuwa kusaidia wanawake na vijana kote ulimwenguni ni muhimu kwa mustakabali wetu wa pamoja, pamoja na elimu, afya, na uwezeshaji katika moyo wa yote," Jill alisema.