"Umenifanya nionekane mjinga!" Mkewe Samidoh amuonya kuhusu uhusiano na Karen Nyamu

Bi Edday alimwambia mumewe kwamba hatakubali kulea watoto katika ndoa ya wake wengi.

Muhtasari

•Edday alimkashifu seneta huyo wa kuteuliwa akimtaja kama mtu asiye na maadili na asiyeheshimu familia yake.

•Edday alidokeza kuwa takriban miaka mitatu iliyopita ya ndoa yake imejawa na maumivu na fedheha nyingi

•Mkewe Samidoh alisema Karen anamzidi umri kwa miaka kumi, sababu nyingine ya kufanya akatae awe mke mwenzake.

Edday Nderitu, Karen Nyamu, Samidoh
Image: HISANI

Mke wa Samidoh, Edday Nderitu amevunja ukimya wake kuhusu drama nyingi zinazozingira ndoa yake ya miaka 15.

Siku moja tu baada ya mwimbaji huyo wa Mugithi kuonekana akiwa na mzazi mwenzake Karen Nyamu, Edday amempa onyo akimjulisha kuwa hayuko tayari kulea watoto wao katika ndoa ya wake wengi.

Kupitia taarifa ya uchungu kwenye ukurasa wake wa Facebook, mama huyo wa watoto watatu alimkashifu seneta huyo wa kuteuliwa akimtaja kama mtu asiye na maadili na asiyeheshimu familia yake.

"Nimemuomba Mungu kila siku anipe nguvu ya kukuombea lakini leo sina la kumwambia Mungu juu yako, umeniburuta na kuniweka mimi na watoto wangu kwenye bahari ya uchungu upate kukumbuka hili," Edday alimwandikia Samidoh.

Edday alidokeza kuwa takriban miaka mitatu iliyopita ya ndoa yake imejawa na maumivu na fedheha nyingi. Licha ya yote, anasema, amebaki mwaminifu na ameendelea kuunga mkono kazi ya mwanamuziki huyo.

"Nimebaki mwaminifu kwako bila kujali kudharauliwa, kudhalilishwa na kutukanwa kwenye mitandao ya kijamii, umenifanya nionekane mjinga na kuchukulia ukimya wangu kuwa wa kawaida, nimekusaidia kuinua kipaji chako na kukuunga mkono kwa yote, lakini kitu kimoja nimekwambia na nasema hapa tena sitalea watoto wangu katika familia ya wake wengi," alisema kwa uchungu.

Edday alidai kuwa mzazi mwenza wa mumewe anamzidi umri kwa miaka kumi, sababu nyingine ya kufanya akatae awe mke mwenzake.

Alibainisha kuwa ndoa yake ilikuwa nzuri siku za awali kabla ya mtu wa tatu kuingia ndani yake takriban miaka mitatu iliyopita.

"Imekuwa miaka 15 kamili ya ndoa iliyojaa panda shuka, ilikuwa mwanzo mdogo ambapo kidogo ilikuwa ya kutosha kwetu, kwa miaka mitatu iliyopita imekuwa maumivu,"

Seneta  Karen Nyamu na  Samidoh walikuwa miongoni mwa wageni waliohudhuria hafla ya mazishi ya shemeji wa naibu rais Rigathi Gachagua, Nancy Muthoni katika eneo la Gatanga, kaunti ya Murang'a siku ya Alhamisi.

Baadaye jioni, Bi Nyamu alichapisha picha kadhaa  za hafla hiyo kwenye kurasa zake mbalimbali za mitandao ya kijamii.

Katika taarifa yake, wakili huyo alibainisha kuwa alikuwa amehudhuria ili kufariji familia ya naibu rais.

"Leo nimefariji familia ya naibu rais Rigathi Gachagua kufuatia kifo cha shemeji yake Nancy Muthoni. Alizikwa katika Kijiji cha Kamunyaka, Eneobunge la Gatanga, Kaunti ya Murang'a," aliandika kwenye Facebook.

Kati ya picha alizochapisha ni pamoja na moja ya mzazi mwenzake Samidoh akitoa hotuba yake kwenye hafla hiyo na nyingine inayoonyesha wakiwa wamekaa karibu na kuonekana kufurahia muda pamoja.