Hisia baada ya Karen Nyamu kukutana na Samidoh katika kaunti yake ya nyumbani

Wawili hao wanadaiwa kukutana kwenye kikao kimoja katika ofisi ya gavana Badilisha.

Muhtasari

•Samidoh alisema walijadiliana na gavana kuhusu namna sanaa inavyoweza kutumika kukuza utalii katika kaunti hiyo.

•Karen alisema alishiriki majadiliano na gavana kuhusu jinsi sekta ya utalii ya Nyandarua inaweza kufanyiwa marekebisho.

Samidoh na Karen Nyamu
Image: HISANI

Seneta wa kuteuliwa Karen Nyamu na mzazi mwenzake Samuel Muchoki almaarufu Samidoh wanadaiwa kukutana katika kikao kimoja siku ya Ijumaa.

Katika kurasa zao za mtandao wa Facebook, wapenzi hao wawili wa zamani walichapisha taarifa ya mkutano na gavana wa kaunti ya Nyandarua, Dkt Kiarie Badilisha ambao wote walihudhuria katika afisi zake.

Samidoh alisema walijadiliana na gavana kuhusu namna sanaa inavyoweza kutumika kukuza utalii katika kaunti hiyo.

"Asante Mhe Dkt Kiarie Badilisha kwa nafasi kwa vijana kutoa mawazo yao. Tunatarajia kuona utekelezaji ukifanyika," alisema.

akizungumza wakati wa mkutano na gavana Kiarie Badilisha
Samidoh akizungumza wakati wa mkutano na gavana Kiarie Badilisha
Image: FACEBOOK// SAMIDOH

Staa huyo wa Mugithi ambaye pia ni afisa wa polisi ni mzaliwa wa Ol Jorok ambayo iko katika kaunti hiyo wa eneo la kati.

Kwa upande wake, Karen alisema alishiriki majadiliano na gavana kuhusu jinsi sekta ya utalii ya Nyandarua inaweza kufanyiwa marekebisho.

"Leo nimemtembelea gavana wa kaunti ya Nyandarua, Mheshimiwa Dkt Badilisha Kiarie ofisini kwake. Tulijadili maono yake ya kurekebisha sekta ya utalii na kuweka Nyandarua kama sehemu muhimu ya mzunguko wa utalii nchini Kenya kwa watalii wa ndani na wa kimataifa," seneta huyo wa UDA alisema.

Mama huyo wa watoto watatu aliambatanisha taarifa hiyo yake na picha yake na gavana Kiarie Badilisha.

baada ya kukutana na gavana Kiarie Badilisha.
Karen Nyamu baada ya kukutana na gavana Kiarie Badilisha.
Image: FACEBOOK// KAREN NYAMU

Karen Nyamu na Samidoh hata hivyo hawakuthibitisha kama kwamba walikuwa kwenye kikao kimoja ama walikutana na gavana katika nyakati tofauti. Pia hakuna picha yoyote kuthibitisha kwamba walikutana.

Baadhi ya wanamitandao ambao walitoa maoni chini ya chapisho zao hata hivyo walisisitiza kuwa wawili hao walikuwa kwenye kikao kimoja.

Tazama baadhi ya maoni ya wanamitandao:-

Nancy Gabriel: Mlikuwa kijijini acha uwongo.

Grace Njengo: Kuna picha hujapost

Rozzy Gabriel: Nyinyi ni kama hamwachani wacha nikaskie vibaya na huko.

Alpha Moh: Karen Nyamu ni mpiga picha mzuri, mimi niko na furaha.

Alex K Githu: Siku moja Nyamu alikuwa huko, Kazi nzuri ni muhimu.