•Gidi alitumia wikendi yake nyumbani kwake kijijini katika kijiji cha Kanyamwa, eneo la Ndiwa katika kaunti ya Homa Bay.
•Gidi alifichua kuwa yeye na mkongwe huyo walizungumza kuhusu Arsenal ambapo alimwambia nafasi yake kushinda kombe la EPL ni finyu sana.
Mtangazaji wa kipindi cha Gidi na Ghost asubuhi kwenye Radio Jambo, Joseph Ogidi almaarufu Gidi alitumia wikendi yake nyumbani kwake kijijini katika kijiji cha Kanyamwa, eneo la Ndiwa katika kaunti ya Homa Bay.
Gidi alishiriki baadhi ya nyakati zake nzuri kijijini kwenye kurasa zake mbalimbali za mitandao ya kijamii.
Siku ya Jumapili, alionyesha picha yake katika Uwanja wa Ndege wa Wilson baada ya kuwasili jijini Nairobi kutoka Nyanza. Katika picha hiyo, alikuwa pamoja na mkongwe maarufu ambaye kwa muda mrefu amekuwa akiburudisha Wakenya kwenye mitandao ya kijamii kwa video zake za kuchekesha
"Leo nimesafiri na nyanya huyu mashuhuri," Gidi alisema chini ya picha hiyo.
Mtangazaji huyo mahiri ambaye ni shabiki sugu wa Arsenal alifichua kuwa yeye na ajuza huyo walizungumza kuhusu klabu hiyo ambapo alimwambia nafasi yake kushinda kombe la EPL ni finyu sana.
"Ananiambia ati Arsenal itashinda ligi yesu akirudi, wueh," alisema.
Haya yanajiri wakati ambapo klabu hiyo yenye maskani yake London inatatizika kukaa kwenye mbio za ubingwa wa EPL.
Wanabunduki ambao wamekuwa kileleni mwa jedwali la EPL kwa muda mrefu zaidi msimu huu wamekosa kushinda mechi zao tatu zilizopita huku zote zikiisha kwa sare. Hii imesababisha ongezeko la uwezekano wa washindani wao wakuu Man City kuwapata kwani pengo kati yao ni pointi tano pekee huku Arsenal wakiwa wamecheza mechi mbili zaidi ya washindi hao wa ligi kuu msimu uliopita.
Katika mechi ya hivi majuzi, siku ya Ijumaa, Arsenal walilazimika kutoka nyuma ili kupata angalau pointi moja kutoka kwa mchuano wake na klabu ya Southampton, ugani Emirates ambao uliishia sare ya 3-3.
Matokeo ya mechi hiyo yalimsikitisha Gidi ambaye alieleza wasiwasi wake kupitia akaunti yake ya Tiktok.
"Mambo imechemka! Lakini tunabaki wanyenyekevu, Mungu mbele," alisema.