Kinuthia afunguka jinsi alivyokataliwa katika nyumba ya kupanga kufuatia madai ya 'kula fare'

Muhtasari

•Kinuthia alisema uvumi uliokuwa unasambazwa ulimfikia alipokuwa anatoka saluni kutengenezwa nywele.

•Mwanavlogu huyo alifichua kuwa kisa hicho kilialika madhara mengi ikiwemo kukataliwa katika nyumba ambayo alikuwa amelipia tayari.

Kelvin Kinuthia katika studio za Radio Jambo
Kelvin Kinuthia katika studio za Radio Jambo
Image: MERCY MUMO

Mwanavlogu Kelvin Kinuthia amefunguka kuhusu kisa cha mwaka jana ambapo alivuma sana baada ya kudaiwa kujifanya mwanadada na kulaghai jamaa zaidi ya shilingi tatu.

Akiwa kwenye mahojiano na Massawe Japanni katika kitengo cha Ilikuaje?, Kinuthia alisisitiza kuwa madai hayo yalikuwa ya uwongo. 

Kinuthia alisema uvumi uliokuwa unasambazwa ulimfikia alipokuwa anatoka saluni kutengenezwa nywele.

"Nilikuwa katika saluni. Dadangu alinipigia simu akaniuliza mbona nimekula fare bila kumgawia. Alinitumia screenshot kwenye WhatsApp .Nilidhani ni wanblogu tu wa kawaida eti hiyo kitu itakuja tu na iishe. Nikitoka saluni nilipata jumbe nyingi kwenye ukurasa wangu wa Instagram nikagundua kuwa ni kitu ambacho kilikuwa kimevuma. Nililazimika kujitokeza kueleza ukweli kwani huo ulikuwa uongo," Kinuthia alisema.

Mwanavlogu huyo alifichua kuwa kisa hicho kilialika madhara mengi ikiwemo kukataliwa katika nyumba ambayo alikuwa amelipia tayari.

Alisema kuwa mmiliki wa nyumba hiyo alimrejeshea pesa zake baada ya kufikiwa na uvumi wa 'kula fare' ambao ulivuma kwa kasi.

"Nilikuwa nimetafuta nyumba ambayo nilitaka kuhamia. Hiyo stori ilitokea takriban siku tano kabla ya wakati ambao nilifaa kuingia. Maagenti wa nyumba walinipigia na kuniambia kuwa mwenye nyumba amesema hawezi kubali stori kama ile iliyokuwa imetokea. Aliniambia kuwa hawezi kumshawishi na atalazimika kurejesha hela zangu," Alisimulia.

Kinuthia alikiri kuwa aliathiriwa na msongo wa mawazo baada ya kukataliwa pale kwani tayari alikuwa ametoa ilani ya kuhama.

Mwanavlogu huyo alisema kuwa wengi walichukulia uvumi huo kuwa kweli kwa kuwa wiki hiyo alikuwa amenunua simu mpya.