Willis Raburu afichua sababu ya kunyoa dreadlocks zake

"Ilikuwa uamuzi tu ambao nilifanya!" alisema.

Muhtasari

•Mtangazaji huyo mwenye umri wa miaka 35 aliweka wazi kwamba hakuwa na sababu maalum ya kuzikata nywele zake.

•Alisema kuwa kuweka dreadlocks hizo  pia ni uamuzi ambao alifanya tu kwani kila mara alitaka kuwa nazo.

Willis Raburu katika studio za Radio Jambo
Image: RADIO JAMBO

Mtumbuizaji wa kipindi cha 10/10 kwenye Citizen TV Willis Raburu amedai kuwa dreadlocks alizonyoa zina thamani ya Ksh45,000.

Katika mahojiano na Massawe Japanni, Raburu alieleza kwamba alikuwa na nywele hizo kwa miaka miwili kabla ya kuzikata.

"Ziko nyumbani. Niliambiwa ni 45,000. Nilikuwa nazo miaka miwili," Raburu alisema katika kipindi cha Bustani la Massawe.

Mtangazaji huyo mwenye umri wa miaka 35 aliweka wazi kwamba hakuwa na sababu maalum ya kuzikata nywele zake.

"Ilikuwa uamuzi tu ambao nilifanya!" alisema.

Alisema kuwa kuweka dreadlocks hizo  pia ni uamuzi ambao alifanya tu kwani kila mara alitaka kuwa nazo.

"Nilipowacha kusoma habari, nilijiambia kuwa nimekuwa nikitaka locks. Nilipigia mchumba wangu wa sasa nikamwambia naenda kuweka locks. Alisema ni sawa. Niliuliza mtaalam ikiwa nywele yangu inaweza kufungwa akasema ndio," alisema.

Mtangazaji huyo aliwashukuru waajiri wake kwa kutompiga kalamu baada ya kubadilisha mtindo wake wa nywele.

"Watu walikuwa wanasema eti sitachukuliwa kwa umakini, nitakosa kupata kazi, nitakosa kupata wadhamini na bibi atanitoroka lakini nikasema kuna watu wenye maarifa ambao wake nao," Raburu alisema na kutoa mifano ya wasanii Nyashinski, Nameless na wakili Bobby Mkangi.

Aliongeza, "Sikuwa nikae nazo sana lakini lazima ningethibitishia watu kuwa unaweza kufanya unachotaka."

Mtumbuizaji huyo alinyoa dreadlocks zake mwezi uliopita na kuweka nywele fupi. Amesema kuwa baadhi ya watu bado wanakosoa mtindo wake mpya wa nywele.