Nuru Okanga afichua jinsi Pasta Ng'ang'a alimtabiria nyota ya kuwa mwanasiasa shupavu

" Aliniambia mambo mawili; wewe hii Kenya utakuwa mwanasiasa mkubwa ama utakuwa nabii kama mimi" Nuru Okanga alisema.

Muhtasari

• Alisema kwamba alilazimika kurudi shule kwa sababu analenga kuwania kama MCA katika kaunti ya Kakamega.

• Alimsifia Pasta Ng’ang’a pakubwa akimtaja kama nabii wa kweli wa Mungu licha ya kwanza watu wengi wanamchukulia kama mchungaji wa hovyo na mwenye utata

Pasta Ng'ang'a na Nuru Okanga
Pasta Ng'ang'a na Nuru Okanga
Image: Maktaba

Mwanasiasa chipukizi ambaye pia ni mtetezi wa sera za Raila Odinga, Nuru Okanga amefichua kwamba ndoto yake ya kuwa mwanasiasa ilitabiriwa miaka mingi nyuma na pasta Ng’ang’a wa kanisa la Neno Evangelical, kabla hata ya mtu yeyote kumfahamu au kumuaminia.

Akizungumza na Massawe Japanni katika stesheni ya Radio Jambo kwenye kitengo cha Ilikuaje, Okanga alisema kwamba aliwahi kuwa mhubiri kabla ya kutoroka kazi za kuchunga mifugo na pia kufanya kazi za mjengo kwenye ujenzi.

Alimsifia Pasta Ng’ang’a pakubwa akimtaja kama nabii wa kweli wa Mungu licha ya kwanza watu wengi wanamchukulia kama mchungaji wa hovyo na mwenye utata mwingi katika mahubiri yake.

Okanga alisimulia kisa kimoja kilichomkutanisha na Pasta Ng’ang’a, wakati ambapo mchungaji huyo alimuita kutoka katikati ya wuamini na kumtabiria kwamba angekuwa mwanasiasa shupavu.

“Pasta Ng’ang’a ni nabii ambaye ameitwa na Mungu. Ng’ang’a akiwa na mkutano katika shule ya msingi ya Dhawabu, sikuwa nimeonana na yeye na hata sikuwa ninajua Ng’ang’a anakaa aje huo wakati. Nilikuwa nimevaa tsheti nyekundu na nilikuwa mbali sana na yeye nikiwa nimevaa kofia ya ODM,” Okanga alikumbuka.

“Ng’ang’a alikuwa na CD 10 kwa mkono, akaamua kuzirusha kwa watu wang’ang’anie. Akabaki na moja mkononi akasema hii moja sirushi, nataka nibariki mtu. Akaniita akaniambia wewe ambaye umevalia kofia ya ODM kuja hapa, nikashtuka kwani huyu mtu ni nini anataka kunifanyia. Akatuma mtu wake enda umlete.”

“Mimi sikuogopa, nikaenda. Aliniambia mambo mawili; wewe hii Kenya utakuwa mwanasiasa mkubwa ama utakuwa nabii kama mimi, na akaniambia chukua hii CD hata kama huna runinga ya kutumia kuitazama, enda uweke kwa nyumba yako italeta Baraka kwako. Na kweli imeleta, mimi ni mwanasiasa mkubwa, ndoto zimetimia kwa sababu kila mahali ukiona mtu anapigana na Deep State bila woga jua huyo ni mtu mkubwa ambaye anafuata maandiko,” alimaliza kwa kunukuu kufungu cha Biblia kuhusu kutoogopa.

Akielezea hadithi yake, Okanga ambaye aligonga vichwa vya habari kwa kufanya KCPE akiwa na miaka 32, alisema kwamba alilazimika kurudi shule kwa sababu analenga kuwania kama MCA katika kaunti ya Kakamega na asingependa kuwa kiongozi ambaye hana cheti chochote cha masomo.

Okanga alisema kwamba aliacha shule akiwa na miaka 6 tu kufuatia kifo cha babake.