Patanisho ya Ma'celeb: Massawe Japanni awapatanisha Milly Chebby na Jackie Matubia hewani (maelezo)

Jackie Matubia alithibitisha urafiki wao kwa kufichua kwamba atahudhuria tamasha la Terence Creative la ‘Wash Wash 4’.

Muhtasari

•Massawe Japanni alifanya hatua kubwa ya kujaribu kuwapatanisha Milly Chebby na rafiki yake Jackie Matubia ambaye inadaiwa walikosana.

•Milly Chebby alibainisha kuwa hawajavunja urafiki wao wa miaka mingi lakini badala yake walikuwa wamechukua kipindi cha mapumziko tu.

aliwapatanisha Milly Chebby na Jackie Matubia.
Massawe Japanni aliwapatanisha Milly Chebby na Jackie Matubia.

Siku ya Alhamisi mchekeshaji, wakati mchekeshaji Terence Creative na mke wake Milly Chebby walipotembelea studio za Radio Jambo, mtangazaji Massawe Japanni alifanya hatua kubwa ya kujaribu kuwapatanisha wanandoa hao mashuhuri na rafiki yao wa muda mrefu Jackie Matubia ambaye inadaiwa walikosana.

Alipokuwa akiwahoji wanandoa hao kuhusu kile kilichojiri wakati wa shoo yake ya Bustani la Massawe, Massawe Japanni alimpigia simu Bi Matubia moja kwa moja hewani na akapokea kwa furaha.

Kisha mtangazaji huyo mwenye sauti ya kupendeza aliendelea kumjulisha muigizaji huyo wa zamani wa Tahidi High kwamba alikusudia kumpatanisha na rafiki yake wa muda mrefu, Milly Chebby.

“Kupatanisha kweli? Imefika hapo kweli?” Jackie Matubia alijibu huku akicheka kwa nguvu.

Kisha Massawe aliendelea kuwataka marafiki hao wawili wa muda mrefu wazungumze wao kwa wao ili kusuluhisha mzozo wao ambao bado haujajulikana.

“Sasa nitamwambia nini jameni?!” Milly Chebby alihoji.

Akizungumza kwa niaba ya mkewe, Terence Creative alikana madai kuwa walikosa kumwalika Bi Matubia kwenye hafla yao ya hapo awali wakidai kuwa hana mume.

Kisha Milly Chebby akarudia swali la mtangazaji Massawe Japanni kwa rafiki yake huyo wa muda mrefu kuhusu kama anam’miss yeye na urafiki wao.

“Mnanifurahisha. Ndio (nam’miss)," alisema.

Huku akijibu kuhusu mzozo wao, Bi Matubia alisema, “Vile walisema, mimi sina ya kuweka ama ya kutoa. Walichosema tu, hivyo ndo iko. We are family, kukosana ni kawaida tu.”

Milly Chebby kwa upande wake alibainisha kuwa hawajavunja urafiki wao wa miaka mingi lakini badala yake walikuwa wamechukua kipindi cha mapumziko tu.

“Si wanadanganya ati tumekosana. Si ni break tu..,” Milly alisema.

Jackie Matubia alithibitisha urafiki wao kwa kufichua kwamba atahudhuria tamasha la Terence Creative la ‘Wash Wash 4’ ambalo limeratibiwa kufanyika Jumatatu, Desemba 11.

“Wasee tujitokeze tu kwa show, tupatane kwa show tutazame Wash Wash, tufurahie alafu turudi kazi.. Ndiyo ninahudhuria shoo,” alisema.

Pia alibainisha kuwa hakuna kitu kibaya kati yake na Milly Chebby ili kudai msamaha.

Terence alimalizia kwa kusema, “So long sisi ni familia kuna kukwaruzana, ambalo ni jambo la kawaida. Jambo ni kwamba, unachukuaje mzozo mlio nao kama familia na unauendeleza kwa kiwango gani."