"Nina wake wengi!" Jay Melody afunguka kuhusu mahusiano yake

Jay Melody ameweka wazi kuwa yeye ni kipenzi cha wengi.

Muhtasari

•"Nina wake wengi. Vipenzi wangu ni wengi. Wanaotupenda ni wengi. Nawapenda wote," Jay Melody alisema.

•Mwimbaji huyo alifunguka kuhusu upendo wake mkubwa kwa watu na wasanii wa Kenya.

Jay Melody na Massawe Japanni
Image: RADIO JAMBO STUDIO

Mwimbaji mAshuhuri wa Bongo Sharrif Said almaarufu Jay Melody ameweka wazi kuwa yeye ni kipenzi cha wengi.

Akizungumza katika mahojiano na mtangazaji Massawe Japanni kwenye Bustani la Massawe, Melody alibainisha kuwa anawapenda wote wanaompenda.

"Nina wake wengi. Vipenzi wangu ni wengi. Wanaotupenda ni wengi. Nawapenda wote," alisema

Mwimbaji huyo alibainisha kwamba, kama vile wasanii wengine wengi, hapendelei kuweka wazi hali yake ya uchumba kwa kuwa anafahamu fika kwamba pindi atakapofanya hilo, basi atakuwa amewavunja moyo wanadada wengi wanaommezea mate.

"Hatutaki kuweka hali yetu kwa sababu tutadisappoint wengi. Wanaonipenda ni wengi. Nawapenda wote," alisema.

Wakati wa kipindi hicho cha Ijumaa adhuhuri, mtangazaji Massawe Japanni alimtania staa huyo wa Bongo iwapo atamchukua mtangazaji wetu wa habari Tina Masika ambaye alionesha kumtaka kuwa mchumba wake.

"Kuna dada yetu hapa, na mwaka huu tumemuamulia," alisema Massawe.

Melody hata hivyo alionekana kupuuzilia ofa hiyo maalum na kupendekeza wengine kwenye timu yake.

Wakati huo huo, mwimbaji huyo alifunguka kuhusu upendo wake mkubwa kwa watu na wasanii wa Kenya.

Mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 25 alisema kwamba anapata msukumo mkubwa kutoka kwa wasanii wengi wa Kenya.

"Nawapenda watu wengi Kenya. Napata msukumo kwa wasanii wa Kenya. Nawapenda kina Otile Brown, Jovial Mejja, Masauti," alisema.

Alisema kuwa nyimbo za Kenya zinachezwa sana nchini Tanzania hasa jijini Dar es Salaam.

Pia alidokeza kuwa atafanya collabo na msanii wa Kenya hivi karibuni.