Jamaa apata nguo za jamaa mwingine kwa nyumba ya mkewe wiki mbili tu baada ya kumfukuza

Muhtasari

•Rael alikiri kwamba mumewe alipomfukuza alienda akatafuta nyumba ya kupanga na kutokana na ghadhabu aliyokuwa nayo akaamua kujitosa kwenye mahusiano na mwanaume mwingine.

•Alisema licha ya mumewe kupata ishara kwamba tayari mwanamume mwingine alikuwa amechukua majukumu yake bado alitaka warudiane.

•Rael alisema mumewe anakabiliwa na msongo wa mawazo kwani anadhani mkewe bado hajakatiza uhusiano wake na mwanamume aliyekuwa naye.

Gidi na Ghost
Gidi na Ghost
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi kitengo cha Patanisho, mwanadada aliyejitambulisha kama Rael kutoka Kisii alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mume wake Daniel Nyangweso ambaye walikosana kufuatia mzozo wa kinyumbani.

Rael alisema ndoa yao ya miaka 10 ilianza kuyumba mwezi Aprili mwaka huu wakati alipokosea mumewe akakasirika na kumfukuza.

Alikiri kwamba mumewe alipomfukuza alienda akatafuta nyumba ya kupanga na kutokana na ghadhabu aliyokuwa nayo akaamua kujitosa kwenye mahusiano na mwanaume mwingine.

"Kuna wakati tulikosana na yeye kwa nyumba. Alikuwa na hasira sana akanitolea vitu nje. Nilijawa na hasira nikatoka nikaenda kuchukua nyumba. Kweli nilimkosea, vile nilichukua nyumba nikawa na mwanamume mwingine. Baada ya kukaa wiki mbili akanitafuta akataka nirudi. Alikuja akapata nguo kwa nyumba akakasirika sana" Rael alisimulia.

Alisema licha ya mumewe kupata ishara kwamba tayari mwanamume mwingine alikuwa amechukua majukumu yake bado alitaka warudiane.

Bwana Daniel alimwambia Rael kuwa alikuwa amejuta kumfukuza nyumbani na kumuomba msamaha huku akimhakikishia kwamba hasira ilikuwa imepungua. Rael hata hivyo alisema baada ya kurudiana mumewe amekuwa na mawazo mengi na hakujakuwa na raha yoyote kwa nyumba.

"Aliniambia tu nirudi tukae na yeye kwani alinikosea  na hasira aliyokuwa nayo ilikuwa imeisha. Tulirudiana ndio lakini raha aliyokuwa nayo hapo awali haipo tena. Huwa anakaa tu na stress kila wakati. Ningependa kumuomba msamaha, tuishi maisha kama tuliyokuwa tunaishi mwanzoni. Ako na stress  sana hata namuonea huruma" Alisema Rael.

Rael alisema mumewe anakabiliwa na msongo wa mawazo kwani anadhani mkewe bado hajakatiza uhusiano wake na mwanamume aliyekuwa naye.

Jaribio la kupatanisha wanandoa hao wawili hata hivyo liligonga mwamba kwani bw Daniel alikuwa amezima simu wakati Gidi alijaribu kumpigia.

Rael hata hivyo alitumia fursa aliyopewa kukiri makosa yake na kumuomba mumewe msamaha huku akimhakikishia kwamba tayari alikuwa amekatiza mahusiano na mwanamume aliyekuwa naye.

"Najua nilikukosea. Ningependa unisamehe sitawahi kurudia tena. Ningependa amani irejee kwa ndoa yetu. Hakuna mtu mzuri, ndoa ni watu kuelewana na kupendana. Usikuwe na stress, mwanamume nilikuwa naye tuliachana na siweze kuwa naye tena. Ilikuwa mambo ya hasira na iliisha" Rael alisema.

Je, una ushauri upi kwa wanandoa hao?