Patanisho: Jamaa ajuta baada ya kuachwa pweke alipofumaniwa na mpango wa kando

Muhtasari

•Onyango alisema mke wake aliondoka na mtoto wao mmoja  wakati alirejea nyumbani mapema kutoka sokoni na kumfumania na mpango wa kando ndani ya nyumba ya ndoa.

•Onyango alisema wakati hayo yote yalikuwa yanaendelea mpango wake wa kando alikuwa ametulia tu kwa nyumba kwani alikuwa amemwagiza asalie mle ndani.

Gidi na Ghost
Gidi na Ghost
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi, jamaa aliyejitambulisha kama Onyango (28) kutoka Ugenya alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Emma (24)  ambaye walikosana mwezi uliopita kuhusiana na suala la mpango wa kando.

Onyango alisema mke wake aliondoka na mtoto wao mmoja  wakati alirejea nyumbani mapema kutoka sokoni na kumfumania na mpango wa kando ndani ya nyumba ya ndoa.

"Bibi alikuwa ameenda kuuza vitu sokoni. Nami nilikuwa nimeitana hapo kwa nyumba sikutarajia anaweza rudi mapema. Aliporudi alinipata na mrembo akiwa ameketi tu kwa kiti. Hakuniongelesha, aliingia tu kwa nyumba alafu akatoka akiwa amekasirika. Nilitoka nikafunga mlango kutoka nje alafu nikamfuata, hakuniongelesha hata akaenda akarudi na mtu wa pikipiki. Kumbe alikuwa ashajipanga, alichukua mfuko wake na akaenda na mtoto mmoja mwenye tulipata na yeye" Onyango alisimulia.

Onyango alisema wakati hayo yote yalikuwa yanaendelea mpango wake wa kando alikuwa ametulia tu kwa nyumba kwani alikuwa amemwagiza asalie mle ndani.

Alisema tayari alikuwa ameachana na mpango wake wa kando baada yao kukosana  ila juhudi zake nyingi za kurejesha mkewe hazikuwa zimefua dafu.

Emma alipopigiwa simu alikubali kusikiza ombi la msamaha la mume wake.

Onyango alimuarifu Emma kuwa amekuwa akiishi katika hali ya upweke tangu alipomuacha huku akimhakikishia kwamba aliacha mambo ya mipango wa kando.

Alimwambia mkewe alikuwa amejuta matendo yake na kuapa hatawahi rudia iwapo angekubali kumrudia.

Emma alisema bado anauguza uchungu ambao mumewe alimsababishia moyoni na anahitaji muda kabla ya kufanya maamuzi ya kurudi. Hata hivyo alikubali kumsamehea.

"Uchungu bado iko. Alikuwa anahanya na mimi bado nilikuwa nyumbani kwake. Hatujakaa sana na yeye, tumekaa miezi mitano. Kama ameacha kuhanya mimi nimemsamehe. Bado nafikiria iwapo nitarudi kwake. Acha huu mwaka uishe" Emma alisema.

Wawili hao walihakikishiana kuwa wangali wanapendana sana .