"Mimi sina haja na yeye!" Jamaa avunjwa moyo baada ya kugundua mkewe ashanyakuliwa na mwingine

Muhtasari

•Morris alisema mke wake aligura ndoa yao ya miaka miwili baada yake kuhusika kwenye ajali na kulazwa hospitalini.

•Alisema ingawa hawajakuwa pamoja kwa miaka mingi bado ana matumaini ya kurudiana kwani kulingana na uchunguzi wake Susan bado hajaolewa kwingine.

•Susan pia alimnyima Morris nafasi ya kuona mtoto wao akilalamika kuwa hajakuwepo miaka mitano ambayo imepita.

Gidi na Ghost
Gidi na Ghost
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi kitengo cha Patanisho jamaa aliyejitambulisha kama Morris alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na aliyekuwa mke wake, Susan, ambaye walitengana miaka mitano iliyopita.

Morris alisema mke wake aligura ndoa yao ya miaka miwili  baada yake kuhusika kwenye ajali na kulazwa hospitalini mnamo mwaka wa 2016.

Aliweka wazi kwamba hakuwa amekosea mkewe kwa namna yoyote wakati alifanya maamuzi ya kutoroka ndoa.

"Nilikuwa nafanya kazi Nairobi nikapata ajali alafu akapigiwa simu na marafiki wakaja na ndugu yangu na dadangu kuniangalia. Alipoenda nyumbani akatoroka. Nilikuwa nimeumia mbavu na miguu lakini nilipona. Saa hii niko sawa hata nafanya kazi. Aliona kwa vile niligonjeka sikuwa na pesa vizuri  za kumlinda. Sikumpiga na hata sikumtukana" Morris alisimulia.

Alisema ingawa hawajakuwa pamoja kwa miaka mingi bado ana matumaini ya kurudiana kwani kulingana na uchunguzi wake Susan bado hajaolewa kwingine.

Pia aliweka wazi kwamba wamekuwa wakiwasiliana ila hawajawahi kupatana ana kwa ana tangu walipotengana.

"Nilimpigia simu akaniambia mara ako nyumbani, mara ako kazi. Kuna dalili anaweza rudi. Vile nafikiria najua hajapata mtu. Niko na imani hajapata mtu mwingine" Morris alisema.

Morris alisema angependa  mkewe arudi kwani kwa sasa anateseka sana maishani.

Susan alipopigiwa simu alimkosoa Morris kwa kukosa kuwajibikia mtoto wao katika kipindi cha miaka mitano ambayo hawajakuwa pamoja.

Susan aliweka wazi kwamba tayari amesonga mbele na maisha yake na hata ana mume ambaye anapanga kufunga ndoa naye.

"Hakuna nafasi. Mimi nishamove on. Niko na mwanaume na hata natarajia kufunga ndoa naye" Susan alisema.

Morris hakutaka kukubali kwamba aliyekuwa mkewe alikuwa anatazamia kuolewa kwingine ilhali wana mtoto pamoja.

"Huyo hajaoleka, ako tu nyumbani" Alisema Morris.

Susan alisisitiza  hataki kamwe kurudiana na Morris "Kwa saa hii mimi sina haja na yeye. Aangalie maisha yake mimi nitalinda mtoto niko na uwezo. Nitamsomesha. Mimi  nimeshamove on, yeye apange maisha yake. Ameoa, ameoa, ameoa. Aishi na hao wenye huwa anaoa. Niko na mume nataka tufunge ndoa naye" Susan alisema.

Susan pia alimnyima Morris nafasi ya kuona mtoto wao akilalamika kuwa hajakuwepo miaka mitano ambayo imepita.