Patanisho: Mwanadada agura ndoa baada ya mama mkwe kukamua ng'ombe wake saa sita usiku

Muhtasari

•Morine alisema ndoa yao ya mwaka mmoja ilisambaratika baada yake kuzozana na mama mkwe kuhusu suala la maziwa. 

•Amos alipopigiwa simu alimwomba Morine ampe muda kwanza afikirie kuhusu suala la kurudi kwake

Gidi na Ghost
Gidi na Ghost
Image: RADIO JAMBO

Morine Halima alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na Amos Mwenda ambaye walikosana naye takriban miaka mitatu iliyopita.

Morine alisema ndoa yao ya mwaka mmoja ilisambaratika baada yake kuzozana na mama mkwe kuhusu suala la maziwa. Alisema alikuwa na ujauzito wa miezi mitano alipokuwa anagura ndoa yake.

Alifichua kwamba mzozo ulitimbuka baada ya mumewe kuamka usiku mmoja na kumpata mamake akikamua ng'ombe wao.

"Hatukuwa tumejenga na tulikuwa na mfugo. Nilikuwa nachunga ng'ombe kisha jioni nazikamua tunagawana na mama mkwe nusu nusu. Nikiamka asubuhi nilikuwa napata ng'ombe zimekamuliwa. Mume wangu aliamka saa sita usiku moja akapata mamake akikamua ng'ombe. Baadae yule mama alinitukana nikaamua kutoka," Morine alisimulia.

Morine alifichua kwamba alijifungua akiwa kwao nyumbani na akapiga hatua ya kumfahamisha mumewe kwa simu.

Amos alipopigiwa simu alimwomba Morine ampe muda kwanza afikirie kuhusu suala la kurudi kwake. Alifichua kwamba tayari ana wake wengine wawili ambao Morine anafahamu kuwahusu.

"Mimi sio wa mke mmoja. Niko na wake wengine wawili. Alikuwa wa tatu lakini akajua kuwaliko na aliwakuta pale.  Shida ni hiyo kukosana na mama. Vile aliona nimekosana na mama naye akaenda. Sio mara yake ya kwanza kuenda. Nilimpea muda kwanza azunguke kidogo ajue vile dunia huwa anaenda," Amos alisema.

Morine alimuomba mumewe msamaha huku akiahidi kutorudia makosa yake. 

Amos alikubali kumsamehe Morine na kuomba apatiwe muda kabla ya kufanya uamuzi wa kurudi kwake.