Patanisho: Jamaa ampiga mkewe mjamzito kwa kuondoka nyumbani bila kumjulisha

Muhtasari

•Achieng' alisema aligura ndoa yake mnamo Januari 1, 2022 baada ya mumewe kumpiga kufuatia hatua yake ya kuondoka nyumbani bila kuacha ujumbe.

•Opiyo alipopigiwa simu alitetea kitendo chake cha kumpiga mumewe huku akidai alifanya vile kutokana na hasira

Gidi na Ghost asubuhi
Gidi na Ghost asubuhi
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost kitengo cha Patanisho, mwanadada aliyejitambulisha kama Judith Achieng' alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mumewe Opiyo ambaye walikosana  naye kufuatia mzozo wa kinyumbani.

Achieng' alisema aligura ndoa yake mnamo Januari 1, 2022 baada ya mumewe kumpiga kufuatia hatua yake ya kuondoka nyumbani bila kuacha ujumbe.

Alisema mumewe alimuoa akiwa na mtoto mwingine ambaye alimwachia mamake nyumbani kwao. Kipindi mumewe alimpiga alikuwa na ujauzito wake wa miezi minne

"Mzee aliamka tu na hakuongea akaenda kazi. Sikumuongelesha kwa sababu ni kama alikuwa na hasira. Nilipokea simu nikaambiwa eti mama alishikwa. Singebaki kwa nyumbakwa sababu mama yangu huwa ananisaidia kulea. Sikuweza kumweleza kwa sababu hakuwa na simu. Nilienda mahali huwa  anafanya kazi na sikumpata," Achieng' alisimulia.

Achieng' aliendelea: "Alinioa na mtoto mwingine. Nilipopigiwa simu nilitoka. Nilimaliza kushughulikia mamangu kitu saa kumi jioni. Kurudi nyumbani nilipata mzee amefunga mlango na kuenda na kifunguo.  Alipouliza  mamake mahali nilienda aliawambiwa eti nilitoka saa tatu ilhali nilitoka saa sita. Alirudi akanipata kwa mlango nikamwambia nilienda nyumbani juu mamangu alishikwa. Hapo akaanza kunipiga. Alinikanyanga na mguu nikasema kama ni hivyo ni heri nirudi kwetu," 

Bi Acheng alifichua kwamba wamekuwa wakizungumza na mumewe ila bado hawajazungumzia suala la kurudiana.

"Ningependa kurudi kwa sababu kushughulikia mimba pekee yangu sio rahisi. Niko na ujauzito wa miezi saba," Alisema.

Opiyo alipopigiwa simu alitetea kitendo chake cha kumpiga mumewe huku akidai alifanya vile kutokana na hasira. Alisema mkewe ana mazoea ya kuenda kwao bila kumfahamisha, tabia ambayo aliomba abadilishe.

"Sikumpiga sana vile anavyoeleza. Mimi nataka tu akitoka aniambie. Siku alitoka alirudi nyumbani usiku ndio maana nilikasirika," Opiyo alisema.

Wawili hao walikubaliana kurudiana na wakahakikishiana kuwa kila mmoja wao atabadili tabia zilizotia doa kwenye ndoa yao.