Patanisho: Jamaa yupo tayari kupeleka ndovu mradi mkewe arudi

Muhtasari

•Mutuma aliahidi kwamba tayari amebadilisha tabia zake mbaya za hapo awali na hata kurejea kanisani.

•Brigid alifichua kwamba mumewe alikuwa amezoea kumpiga mara kwa mara baada ya kukosana

Gidi na Ghost
Gidi na Ghost
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi kitengo cha Patanisho, jamaa aliyejitambulisha kama Martin Mutuma alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mkewe Brigid Mwendwa ambaye walitengana naye takriban miaka miwili iliyopita kufuatia mzozo wa kinyumbani.

Mutuma alifichua walitofautia na mkewe mwaka wa 2019 na kwa kuwa ni mwepesi wa hasira akaondoka mara moja na kukataa kurudi.

Alisema kwamba amekuwa akitia juhudi kubwa za kujaribu kumrejesha mkewe ila bado hajaweza kufua dafu.

"Nilijaribu kutafuta wazee tuongee akasema hataki hayo maneno. Nikijaribu kumwambia kitu, anaanza ugomvi. Niliongea naye jana akaniambia ikiwa nataka kuoa nioe. Alisema atarudi lakini hataki kurudi mapema. Aliniambia niendee mtoto lakini sitaki," Mutuma alisema.

Mutuma aliahidi kwamba tayari amebadilisha tabia zake mbaya za hapo awali na hata kurejea kanisani.

"Ata mimi ni mtu wa kukasirika. Nimejaribu sana mpaka nikaenda kwa kanisa, nilirudi kwa maombi. Nimekubali  watu waseme nimekaliwa, boraniendee bibi yangu. Hata wakiniitisha ndovu nitapeleka'" Alisema.

Brigid alipopigiwa simu alifichua kwamba mumewe alikuwa amezoea kumpiga mara kwa mara baada ya kukosana. Ingawa hakutaka kuzungumza zaidi kwa redio, Brigid hata hivyo alidokeza kuwa huenda akakubali kumrudia Mutuma.

"Anipigie yeye mwenyewe. Huwa ananichapa," Brigid alisema.

Mutuma alimhakikishia mkewe kuwa tayari amerekebisha tabia zake na kuahidi kutomchapa tena iwapo watarudiana.