Patanisho: Jamaa aagiza mkewe mjamzito kuapa mbele ya pasta kwamba hakulala na mwanaume mwingine

Muhtasari

•Irene alieleza kuwa mumewe alimfukuza baada ya kumshtumu kwa kulala na mwanaume mwingine. 

•Peter alisisitiza kuwa njia pekee ambayo yuko tayari kumsamehe mkewe ni ikiwa atakiri mbele ya pasta kwamba hakuwahi kulala na mwanamume huyo. 

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi kitengo cha Patanisho, mwanadada aliyejitambulisha kama Irene Masaa alituma ujumbe akiomba kupatishwa na mumewe Peter Shanzu ambaye walikosana hivi majuzi baada ya kwa ndoa kwa mwaka mmoja.

Irene alieleza kuwa mumewe alimfukuza baada ya kumshtumu kwa kulala na mwanaume mwingine. Alisema kuwa matatizo yalianza kukumba ndoa yake baada ya jamaa fulani kumpigia simu akimwitia kazi Nanyuki.

Irene ambaye kwa sasa ana ujauzito wa miezi mitano alidai kuwa rafikiye mmoja ndiye alimchochea kwa mumewe kuwa ana mahusiano na jamaa ambaye alikuwa amemuahidi kazi. 

"Kuna rafiki yangu ambaye tulikuwa tunaambiana kila kitu. Alijua mengi kuhusu mahusiano yangu, nilikuwa namwambia jinsi bwanangu ananipenda.. Tulijuana na askari fulani kupitia Facebook kisha akaniitia kazi. Nilimwambia rafiki yangu kuwa kuna jamaa ameniitia kazi Nanyuki. Kumbe alikuwa amepata namba ya bwanangu. Nilipoenda akamtumia namba ya jamaa ambaye alikuwa ameniitia kazi. Bwanangu alinipigia simu akaniambia nikae huko akidai kuwa nilienda kufanya usherati. Bwana alinifukuza nikaenda kuishi kivyangu," Irene alisema.

Mwanadada huyo alisema rafiki huyo wake alikuwa na mazoea ya kuchochea wapenzi wake dhidi yake.

"Aliwahi kualiambia mwingine kuwa huwa nakunywa dawa za ukimwi. Ni kama alikuwa anaumwa na jinsi bwanangu alikuwa ananipenda," Alisema.

Irene alifichua kuwa bwanake alipopatiwa namba ya jamaa ambaye alikuwa amemwitia kazi alimpigia simu mara moja akitaka kujua ukweli.

Kulingana na Irene, jamaa huyo hata hivyo alimpatia Peter maneno ya uongo kwa kuwa alikuwa na nia ya kulala naye.

"Jamaa alitaka kulala na mimi nikakataa. Bwanangu alipompigia alianza kumpatia maneno ya uongo. Kutoka hapo akawa amenikasirikia. Nilienda mpaka hospitali na ikathibitishwa kuwa sijalala na mtu," Alisema.

Peter alipopigiwa simu Irene alimhakikishia kuwa hakukubali kushiriki tendo la ndoa na mwanaume huyo

"Nilitaka kukuhakikishia kuwa sikulala na huyo mwanaume. Alikuwa ameniitia kazi. Sijawahi kuenda nje hata siku moja," Alisema.

Peter alisisitiza kuwa njia pekee ambayo yuko tayari kumsamehe mkewe ni ikiwa atakiri mbele ya pasta kwamba hakuwahi kulala na mwanamume huyo. 

"Nitakuja tukae na pasta uape kuwa hukufanya hayo. Nataka ushike Biblia uape kwamba hukulala na mwanaume yeyote," Alisema.

Peter alikanusha madai ya kuwa na mahusiano na rafiki ya mkewe huku akidai kuwa hata hajawahi kufika kwake.

Wawili hao walikubaliana kupatana Jumatatu ijayo ili kusuluhisha mzozo wao mbele ya mhubiri.