"Atafute bwana mwingine, mimi nishapendwa!" Brayo amkataa mwanadada aliyepachika mimba

Muhtasari

•Risper alisema ndoa yao ya mwaka mmoja ilivunjika mwezi Machi mwaka jana kufuatia mzozo wa pesa za kliniki.

•Brian alidai kuwa alikuwa ameshinikizwa kwa ndoa yake ya mwaka mmoja na Risper kinyume na mapenzi yake.

Gidi na Gost asubuhi
Gidi na Gost asubuhi
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi kitengo cha Patanisho, mwanadada aliyejitambulisha kama Risper Chemutai (24)  alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mpenzi wake Brian Cheruiyot. (25)

Risper alisema ndoa yao ya mwaka mmoja ilivunjika mwezi Machi mwaka jana kufuatia mzozo wa pesa za kliniki. 

Mwanadada huyo pia alimshtumu mumewe kwa kumfuatilia sana na kutishia maisha yake. Alisema kuwa wakati aligura ndoa yake alikuwa na ujauzito wa miezi miwili.

"Alikuwa ananikazia maisha. Nikitaka kuenda mtoni alikuwa ananikataza. Mtu akinisalimia kwa njia alikuwa ananigombanisha. Hata mama akinipigia simu alikuwa anapaza sauti anamwambia aache kunipigia. Alikuwa ananishikia panga na kunitishia hadi sikuwa nalala usiku. Hapo nikaamue kutoka huko," Risper alisimulia.

Risper alifichua kuwa alijifungua baada ya kugura ndoa yake na kuweka wazi kuwa mumewe amekuwa akishughulikia mtoto licha ya kutengana.

Brian alipopigiwa simu alisema hayuko tayari kurejesha mahusiano yake na Risper. Alisema walizozana kuhusu masuala mengi na tayari ashapiga hatua ya kuoa mwanamke mwingine.

"Mimi nishaoa. Nilipata mwingine. Kusameheana tushasameheana lakini kurudiana mimi nishaoa," Brian alisema.

Brian alidai kuwa alikuwa ameshinikizwa kwa ndoa yake ya mwaka mmoja na Risper kinyume na mapenzi yake. Alisistiza kuwa tayari alikuwa na mwanadada mwingine aliyependa zaidi na ambaye alikuwa ameahidi kuoa.

"Nishampenda mwingine ambaye anaitwa Sharon. Alikuwa mpenzi wangu wa kunitembelea kisha anaenda. Baada ya watoto kumuona siku kadhaa wakanisihi tukae naye tufanye kazi maisha iendelee. Upande wangu kuna ambaye nilimpenda na nikamwambia atakuwa bibi yangu na sasa amekuwa," Alisema.

Brian alisema ni vigumu kuelewana na mke huyo wake wa zamani huku akimshauri atafute mume mwingine.