Patanisho: "Mapenzi yangu kwake yaliisha, sijui shida ni nini!" Mwanadada afungua roho kuhusu mumewe

Muhtasari

•Alex alisema mkewe alianza kuenda nje ya ndoa na hatimaye akagura na kumuachia mtoto wao wa mwaka mmoja.

•Faith alisema kwamba kwa sasa haja na Alex huku akiweka wazi kwamba mapenzi yake kwake yaliisha mara moja.

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi kitengo cha Patanisho, jamaa aliyejitambulisha kama Alex Ateya  alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mkewe Faith ambaye walikosana naye mwaka jana.

Alex alisema masaibu yalianza kukumba ndoa yao baada yake kupata kazi mbali na nyumbani. Alieleza kwamba alipoondoka mkewe alianza kuenda nje ya ndoa na hatimaye akagura na kumwachia mtoto wao wa mwaka mmoja. 

"Hapo awali tuliishi naye vizuri lakini nikapata kazi mahali karibu na mahali mamake ameolewa. Nilipoenda alianza kutembea nje ya ndoa na kila nilipouliza alikuwa ananidanya. Mnamo Desemba 26 nilipata kama ameenda," Alex alisema.

Alex alisema wamekuwa wakiwasiliana na mkewe mara kwa mara katika juhudi za kurejesha uhusiano wao. Hata hivyo hawajaweza kuelewana. 

Faith alipopigiwa simu alifichua kuwa bado ana miaka 18 na kudai kwamba hayuko tayari kutulia katika ndoa. Alisema kwamba kwa sasa anataka kufanya kazi kwanza kabla ya kufanya maamuzi ya ndoa.

"Mimi sirudi. Nilikwambia ujipange. Nipe muda nifikirie. Niko kazini, nataka kusaidie wazazi wangu kwanza kabla nitulie katika ndoa. Kama Mungu amepanga tukae pamoja nitarudi," Alisema.

Faith aliweka wazi kuwa kwa sasa haja na Alex huku akiweka wazi kwamba mapenzi yake kwake yaliisha mara moja.

"Roho yangu iliisha kwake, sijui shida ni nini. Kama ako na haraka na maisha basi ajipange," Faith alisema.

Alisema atafikiria iwapo ataenda kumchukua mtoto wake ama ataacha mamake Alex aendelee kuishi naye.

Alex alisema kwamba yuko tayari kusubiri mpaka wakati mkewe atakubali kurudi nyumbani.