Patanisho: Mtoto afariki baada ya babake kusema "wacha alilie hapo akufe tutaenda kuzika!"

Sharon alifichua matukio ya kushangaza ya kabla ya mtoto wao kufariki ambayo anaamini huenda yalisababisha kifo chake.

Muhtasari

•Sharon alisema ndoa yake ya miezi mitatu ilianza kuyumba mwaka jana baada ya kumzika mtoto wao wa miezi mitatu.

•Sharon alisisitiza kuwa licha ya yote angependa kurudi katika ndoa yake kwani hana mahali kwingine pa kwenda.

Mtangazaji Gidi Ogidi

Bi Sharon Adhiambo ,25,  kutoka Busia alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mume wake Elikana Koech ,29, ambaye alikosana naye mwezi Februari mwaka huu kufuatia kifo cha mtoto wao mdogo.

Sharon alisema ndoa yake ya miezi mitatu ilianza kuyumba mwaka jana baada ya kumzika mtoto wao wa miezi mitatu.

"Ilikuwa ni mwaka huu ambapo tulikosana na mume wangu. Tulizika mtoto wetu wa  miezi mitatu mwaka jana mwezi wa nane, baada ya hapo mambo hayakuwa rais. Nikaamua kuenda kukaa kwa kaka zangu Eldoret. Baada ya katulia, kidogo kidogo nikapigiwa simu nikaitiwa kazi Mombasa," Sharon alisimulia.

Sharon alisema kazi ambayo alikuwa ameitwa kufanya Mombasa imeisha na sasa angetamani kurudi kwa ndoa yake.

Alifichua kwamba baada ya mtoto wao kuaga Bw Koech alianza kisirani kwa nyumba, jambo ambalo lilipelekea yeye kutoroka.

"Wakati tulipoteza mtoto alianza kisirani. Alisema nimejidunga vitu zingine siwezi kupata mtoto. Tulijaribu kupata mtoto mwingine ikashindikana.

Kaka yake alikuwa ananitukana juzi. Alinitumia ujumbe wa matusi kwenye Facebook akisema siwezi kuzaa. Naona yeye ndiye anamchochea nisirudi huko. Mimi sikufanya kitu kibaya. Nilimuachia ndugu yake mkubwa mtoto na sikuwa na ubaya. Huwa nampigia simu kama Jumapili tunaongea na mtoto," alisema

Aliongeza, "Juzi nilimwambia niko mgonjwa niko hospitali ili kupima imani yake. Nilimwambia nilipatikana nimezirai, kumdanganya tu akaniambia nisijali nitapona."

Sharon pia alifichua matukio ya kushangaza ya kabla ya mtoto wao kufariki ambayo anaamini huenda yalisababisha kifo hicho.

"Kabla mtoto akufe kuna maneno alisema ambayo sijawahi kuambia hata watu wetu. Nilimwambia anishikie mtoto ili nifanye usafi akaniambia wacha alilie hapo akufe tutaenda kuzika. Ilikuwa Alhamisi, Ijumaa nikampeleka mtoto kliniki akawa analia tu. Nikaambiwa nimpeleka hospitali ya watoto,.. mtoto kuangaliwa tumboni nikaambiwa ni kama  ako na pneumonia. Nikalazwa pamoja na mtoto juu hakuwa sawa. Mume wangu hakuja kuniangalia hospitali, nikakaa hospitali na mtoto pekee yangu alafu siku ya Jumamosi mtoto akaaga," Sharon alisimulia.

Sharon alisisitiza kuwa licha ya yote angependa kurudi katika ndoa yake kwani hana mahali kwingine pa kwenda.

Alidai kwamba huenda ndugu mkubwa wa Koech huenda anamchochea mume huyo wake asimrejeshe nyumbani.

"Kuna pesa alipata hii mwaka alipewa za loan. Nashuku wanampenda kwa sababu kuna pesa alipata. Akiishiwa  ni hivyo tu anatupwa. Hawana mama na hawana baba, ni yeye tu, ndugu yake mkubwa na mwingine mdogo ambaye yuko shuleni.Ni watu ambao wanatumia mihadarati," alisema Sharon.

Kwa bahati mbaya Bw Koech alipotafutwa kwa simu ili kupatanishwa na mumewe hakupatikana kwani alikuwa amezima.

Sharon alipopewa fursa ya kuzungumza naye hewani alisema, "Iwapo ananiskia, yeye ndiye  alinikosea na nilimsamehe. Pia yeye anisamehe ningependa kurudi kwangu. Nampenda sana na mtoto wangu."

Je, ungemshauri vipi Bi Sharon?