Patanisho:"Simjui, sijawahi kuolewa!" Jamaa arukwa na aliyedai alikuwa mke wake kwa mwaka mmoja

"Mimi ata nishawahi kuolewa? Huyo ametumia bangi asubuhi na sijui imempeleka aje. Mimi sijawahi kuolewa!" Maureen alifoka.

Muhtasari

•Gidi alipopiga simu, aliyechukua ni mwanadada ambaye alijitambulisha kama Maureen na akakana waziwazi kumjua Joseph.

•Joseph ambaye alisikika kushangazwa sana na mazungumzo ya mwanadada huyo na akasisitiza kuwa ni aliyekuwa mkewe.

Image: RADIO JAMBO

Jamaa aliyejitambulisha kama Joseph Muma (31) kutoka Kajiado alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Maryanne Kimundo mwenye umri wa miaka 26 ambaye alikosana naye mwezi Mei mwaka huu.

Joseph alidai kwamba ndoa yake ya mwaka mmoja ilivurugika baada ya mkewe kuanza kushuku alikuwa na mpango wa kando, kosa ambalo alikiri alitenda.

Alijitetea kwa kusema alijipata katika majaribu ya kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanamke ambaye alikuja kujua baadaye alikuwa ameolewa.

"Mpango wa kando alikuwa ni mtu alikuwa ameolewa. Singeweza kukaa na yeye. Nilikuja kujua baadaye.Tulikuwa tumekaa naye mwaka moja. Nilikuwa namshuku sana. Ilifika mahali nikaona kama alikuwa na mimba lakini hakuwa ananiambia," Joseph alisema.

Wakati Gidi alipopiga namba ambayo Joseph alipeana akidai ni ya Maryanne, aliyechukua ni mwanadada ambaye alijitambulisha kama Maureen na akakana waziwazi kumjua Joseph.

"Mimi ata nishawahi kuolewa?  Huyo ametumia bangi asubuhi na sijui imempeleka aje. Mimi sijawahi kuolewa!" Maureen alisema.

Aliongeza, "Simjui. Mimi ata sijawahi kuolewa. Mimi niko 21. Hajawahi hata kuniona."

Joseph ambaye alisikika kushangazwa sana na mazungumzo ya mwanadada huyo na akasisitiza kuwa ni aliyekuwa mkewe.

Alijaribu sana kumsihi mwanadada huyo kuacha kumkana hadharani na kueleza ni nini kilichokuwa kikiendelea.

"Babe, what is going on? .. Tulikuwa tumeoana.Tumekaa na yeye Nairobi, Kayole," Joseph alisema.

Maureen alisema, "Mimi sio msichana wako, hata sikujui. Mimi nilienda Kayole lini?"

Dadake Maureen alibainisha kuwa bado yeye ni msichana mdogo ambaye hajawahi kuolewa.

Joseph alikiri kufadhaishwa sana na matukio yaliyotokea na kuweka wazi kwamba ni mara yake ya kwanza kuumizwa roho.

"Bado sijawahi kuachwa. Huyo ni wa kwanza kuniacha.. Maryanne mimi bado nakupenda," alisema.

Maureen alimwambia, "Aachane na tabia mbaya. Sio kutafuta wrong number. Namjua aje? Amenifanyia vibaya na najihisi vibaya."