Patanisho:"Wanasiasa ni vichwa ngumu!" Gidi azungumzia kuwapatanisha Raila na Ruto

Mtangazaji huyo mahiri alisema kuwa wanasiasa ni wakaidi na wanaweza kumpa wakati mgumu.

Muhtasari

•Gidi ambaye amekuwa akisaidia kuwapatanisha Wakenya waliokosana katika kipindi cha asubuhi kwa zaidi ya muongo mmoja alibainisha kuwa hawezi kushughulika na wanasiasa.

•Ombi la kuwapatanisha Ruto na Raila linajiri wakati ambapo kiongozi huyo wa ODM anaongoza maandamano ya kitaifa dhidi ya serikali.

pamoja na rais William Ruto na Raila Odinga katika picha za maktaba
Gidi pamoja na rais William Ruto na Raila Odinga katika picha za maktaba

Alhamisi asubuhi, mtangazaji wa kipindi cha Gidi na Ghost Asubuhi kwenye Radio Jambo Gidi Ogidi aliombwa kusaidia katika kuwapatanisha Rais William Ruto na kiongozi wa Azimio la Umoja-One Raila Odinga kama jinsi amekuwa akiwapatanisha Wakenya katika kitengo cha Patanisho.

Shabiki mmoja ambaye aliyekuwa akitoa maoni yake kuhusu Patanisho ya Jumatano asubuhi alimbainishia mtangazaji huyo mahiri kwamba ana kila kinachohitajika kuwaleta pamoja wanasiasa hao wawili wakuu wanaozozana na kuwasaidia kuelewana.

“Gidi, hii kazi unafanya, si utafute huyo Raila na Ruto uwapatanishe . Naona wewe unawezana nao, hicho ni kipawa chako,” Hardson Mambili kutoka Westlands alisema.

Katika majibu yake, Gidi ambaye amekuwa akisaidia kuwapatanisha Wakenya waliokosana katika kipindi cha asubuhi kwa zaidi ya muongo mmoja alibainisha kuwa hawezi kushughulika na wanasiasa.

Mwanamuziki huyo wa zamani alisema kuwa wanasiasa ni wakaidi na wanaweza kumpa wakati mgumu.

“Mimi siwezani na wanasiasa, ni vichwa ngumu sana. Wanasiasa ni vichwa ngumu sana,” Gidi alisema.

Aliongeza kuwa angetaka kuendelea kuwapatanisha raia wa kawaida kuliko kushughulika na wanasiasa ambao alisema ni wabinafsi.

“Wacha nishughulike na wananchi wa kawaida. Kuweka wawili chini waongee, vichwa ngumu. Na wana kiburi, kila mmoja ana kiburi,” alisema.

Kwa miaka mingi, Gidi na mtangazaji mwenzake Jacob Ghost Mulee wamekuwa wakiwasaidia Wakenya ambao wamekosana kupatana na kujenga upya uhusiano mzuri. Mara nyingi, watu ambao walikuwa wametofautiana hukubali kusuluhisha tofauti zao katika kitengo cha Patanisho kijacho asubuhi ya kila Jumatatu hadi Ijumaa lakini wakati mwingine inakuwa vigumu kwa wengine kupatana.

Ombi la kuwapatanisha Ruto na Raila linajiri wakati ambapo kiongozi huyo wa ODM anaongoza maandamano ya kitaifa dhidi ya serikali.

Wiki jana, Raila alitangaza kuwa maandamano ya kila wiki dhidi ya serikali ya Ruto yatakuwa yakifanyika kila Jumatano, Alhamisi na Ijumaa. Aliwaomba wafuasi wake kujitokeza mitaani katika siku hizo tatu za juma kuanzia wiki hii.