Kenya yajitenga na uchochezi wa mbunge wa Starehe, Jaguar dhidi ya wageni

JAG
JAG
Serikali imejitenga na matamshi ya mbunge wa Starehe Charles Kanyi, kwa jina la utani Jaguar, dhidi ya raia wa kigeni wanaofanya biashara nchini Kenya.

Katika taarifa yake siku ya Jumatano, serikali ilisema hatua ya mbunge huyo kutumia visivyo uhuru wa kujieleza kuzua uchochezi dhidi ya raia wa kigeni wanaofanyakazi nchini inahujumu utamaduni wa wakenya kuwapokea na kuishi vyema na wageni.

Jaquar alinaswa kwenye video ambayo imekuwa ikizunguka mitandaoni, akiwataka wageni wanoendesha biashara katikati mwa jiji la Nairobi eneo bunge lake, kuondoka au wafurushwe kwa lazima.

Mbunge huyo akiandamana na wafuasi wake, alikuwa ametishia kuvamia maduka ya raia wa kigeni na kuwasafurusha hadi uwanja wa ndege ili warejeshwe makwao. Lakini waziri wa mashauri ya nchi za kigeni Monica Juma amesema matamshi hayo ni ya kusikitisha na yanachochea umma.

Aliongeza kuwa, "Tunachukuwa fursa hii kuwahakikishia raia wote wa kigeni wanaoishi na kufanya kazi Kenya kuwa wako salama na mali yao nchini Kenya italindwa".